Na Göktuğ Çalışkan
Katika Pembe ya Afrika, lugha ya ushirikiano inaandikwa upya kupitia miundombinu.
Bandari, misheni za mafunzo, korido za nishati, na sasa mradi wa kituo cha anga vinaungana kuunda sentensi moja ya kimkakati: uwepo unaozalisha uwezo.
Mpango wa kituo cha anga cha Somalia unapaswa kuangaliwa katika muktadha huu. Kile kinachoonekana mwanzoni kama uwekezaji mdogo wa anga na sayansi, kinageuka kuwa jaribio la kimkakati uliokomaa.
Swali ni kama taifa linaweza kubadili mlango wa diplomasia kuwa msukumo wa kujenga viwanda, na kama ushirikiano wa kiusalama unaweza kukua na kuwa jukwaa la ushirikiano wa teknolojia wa muda mrefu.
Faida ya kijiografia ya Somalia
Mradi ulihama kutoka kuwa ndoto hadi kuingia kwenye ratiba ya utendakazi wa Uturuki na awamu ya kwanza ya ujenzi ilitangazwa hadharani.
Hili ni muhimu kwa sababu miradi ya anga mara chache hushindwa kwa kukosa maono; hushindwa pale ambapo vifaa, ufadhili, na uvumilivu wa kisiasa haviwezi kustahimili safari ndefu ya utekelezaji.
Faida ya Somalia ni wazi na isiyobadilika: eneo lake. Operesheni za kurusha vyombo vya anga hupendelea nchi zinazoweza kutoa njia salama juu ya bahari wazi, hali ya hewa inayotabirika, na ukaribu na ikweta. Katika dunia ambayo kila ongezeko dogo la ufanisi hubadilisha mzigo wa uchumi, jiografia hugeuka kuwa mkakati.
Kwa vitendo, Uturuki inapata aina mpya ya ufikiaji. Mantiki ya kimkakati inajulikana kwa mataifa yenye uwezo wa anga; uzoefu wa Ulaya huko Kourou unaonyesha jinsi eneo la kituo cha anga kijiografia inaweza kubadilishwa kuwa uwezo wa muda mrefu.
Ndiyo maana pia mradi umeundwa kuwa wa awamu tatu. Hii inaashiria nidhamu ya kitaasisi, hupunguza mabadiliko ya kisiasa, vifaa na huruhusu mfumo mzima, kujengwa hatua kwa hatua badala ya kuporomoka chini ya ahadi moja kubwa kupita kiasi.
Uwekezaji wa Uturuki nchini Somalia ni mwendelezo wa mkakati wake wa ushirikiano barani Afrika.
Zaidi ya ushirikiano wa kiteknolojia
Uhusiano kati ya Somalia na Uturuki una sura dhahiri ya kiusalama, na historia hiyo inaupa wazo la kituo cha anga msingi wa kisiasa. Nchi inapotoa mafunzo, kuandaa, na kusaidia kupanga upya miundo ya usalama, hujenga imani isiyoweza kuigwa na ziara fupi au taarifa kwa vyombo vya habari.
Misheni ya muda mrefu ya mafunzo ya kijeshi katika TURKSOM—inayoendelea tangu 2017—ina umuhimu hapa kwa sababu moja: inaonyesha mwendelezo.
Diplomasia ya teknolojia hufanya kazi pale mshirika anapoamini kuwa uhusiano huo utaendelea licha ya misukosuko ya hapa na pale. Kituo cha anga, kwa asili yake, ni dau la muda mrefu. Inahitaji uaminifu wa kisiasa unaothibitishwa kwa miaka, si kutangazwa kwa wiki moja.
Hapa ndipo pendekezo la Uturuki linapojitofautisha katika soko lenye ushindani mkubwa wa ushirikiano barani Afrika. Bara limeona matoleo mengi ya nje yanayoishia kwenye uchimbaji, ununuzi, au suluhisho za muda mfupi za kiusalama. Kituo cha anga ni tofauti kimuundo.
Mradi huu unatoa faida ya elimu, uhandisi, udhibiti, na minyororo ya ugavi katika mzunguko mmoja. Unageuza mahusiano ya mataifa mawili kuwa jukwaa ambalo wadau wengine lazima walizingatie katika mipango yao ya kikanda.
Mradi huu nchini Somalia utavutia umakini kwa sababu inaunganisha hadhi, matarajio ya mapato, na ishara ya kimkakati katika eneo moja. Mpinzani yeyote anayetaka kudhoofisha mamlaka ya dola ataelewa thamani ya kuvuruga mradi unaowakilisha mustakbali wa siku zijazo.
Kwa hiyo, usalama unakuwa sehemu ya muundo wa mradi.
Faida ya Uturuki ni kwamba haianzi kutoka sifuri. Majadiliano ya kituo cha anga yamejengeka ndani ya mpango mpana wa ushirikiano unaojumuisha uratibu wa usalama na teknolojia zinazoibuka—mfumo uliothibitishwa tena katika ngazi ya uongozi na kuripotiwa kama upanuzi wa ushirikiano wa pande mbili hadi sekta ya anga.
Faida ya kituo cha anga
Anga si eneo la anasa tena. Linageuka kuwa tabaka la viwanda linalosaidia mawasiliano, ufuatiliaji wa kilimo, majibu ya majanga, ramani, uangalizi wa bahari, na mipango ya usalama. Kwa nchi zinazoweza kutoa huduma za kuaminika za anga, faida si ya ishara tu; ni ya kibiashara.
Tathmini za karibuni zimeelezea tayari upanuzi wa uchumi wa anga duniani na ukubwa wa soko unaolengwa na Uturuki, ikiwemo makadirio yanayofikia dola trilioni 1.8 ifikapo mwaka wa 2030. Iwe mtu anayaangalia makadirio haya kwa matumaini au tahadhari, mwelekeo ni wazi: mahitaji yanaongezeka, uwezo wa kurusha ni wa kimkakati, na wanaoingia kuchelewa wanahitaji kitu cha kujitofautisha.
Somalia inaweza kuwa kitofautishi hicho ikiwa mradi utachukuliwa kama mfumo wa kikanda badala ya kituo kimoja. Simulizi yenye nguvu zaidi si kwamba “Uturuki inarusha setilaiti zake mwenyewe.”
Bali ni “Uturuki inasaidia kuunda kituo cha anga Afrika inayofundisha vipaji, kujenga minyororo ya matengenezo, na kutoa huduma kwa washirika.” Ikiwa hilo litatimia, mradi utakuwa na msingi wa kiuchumi na uthabiti wa kisiasa.
Kuna pia faida ya nguvu laini (soft power), uwezo wa nchi wa kuvutia au kushawishi wengine bila ya kutumia nguvu, ambayo haipaswi kudharauliwa. Kwa Somalia, kuwa mwenyeji wa miundombinu ya hali ya juu kunaweza kubadilisha simulizi kutoka mgogoro wa kudumu hadi uwezo wa kujenga mustakabali. Kwa Uturuki, kunapanua ajenda ya kitaifa ya anga zaidi ya mipaka ya kijiografia na kugeuza ushirikiano wa Afrika kuwa ubunifu unaoonekana—unatambuliwa na vijana, wahandisi, na wawekezaji, na kuunganishwa na mfumo mpana wa mawasiliano ya setilaiti unaoongozwa na TÜRKSAT.
Jinsi ya kufanikisha
Ili mpango huu udumu kwa muda mrefu, suala la vifaa (hardware) si suala gumu. Kazi ngumu zaidi ni uaminifu. Utawala lazima uwe wazi kiasi cha kuwashawishi wadhamini wa kimataifa, si wanasiasa wa ndani pekee.
Kisha kuna pengo la vipaji. Kituo cha anga kinachoendeshwa kikamilifu na wataalamu wa kigeni haitoshi; kwa uhuru wa kweli, wahandisi wa Kisomali wanapaswa kushika funguo, si kuwa watazamaji tu. Mwisho, suala la usalama lazima lipawe kipaumbele. Katika eneo ambapo hatari hutokea wakati wowote, ulinzi lazima uwe na uwezo wa kubadilika kama teknolojia yenyewe.
Masharti haya yakitimia, kituo cha anga ya Somalia kitakua zaidi ya kichwa cha habari cha mataifa mawili. Itaashiria ukomavu wa diplomasia ya teknolojia ya Uturuki barani Afrika: ushawishi uliojengwa ndani ya vifaa, ujuzi, na taasisi—kisha kulindwa kupitia ushirikiano badala ya misimamo ya kujionyesha.
Mwandishi, Göktuğ Çalışkan, ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) na mtaalamu wa Mahusiano ya Kimataifa.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi misimamo, mitazamo au sera za uhariri za TRT Afrika.




















