Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ameonyesha heshima zake kwa kiongozi wa upinzani wa Kenya, Raila Odinga, aliyefariki nchini India mapema wiki hii na anatarajiwa kuzikwa Jumapili.
Obama alimuelezea Odinga kama kiongozi ambaye "aliweka maslahi ya nchi yake mbele ya matamanio yake binafsi."
Rais huyo wa zamani wa Marekani, ambaye baba yake alitoka Kaunti ya Siaya kando ya Ziwa Victoria - eneo lile lile ambako Odinga alizaliwa na atapumzishwa, alikumbuka kujitolea kwa Odinga kwa maisha yake yote katika kupigania uhuru na demokrasia.
"Raila Odinga alikuwa bingwa wa kweli wa demokrasia. Mtoto wa enzi ya uhuru, alivumilia miongo ya mapambano na kujitolea kwa ajili ya lengo kubwa la uhuru na kujitawala kwa Kenya," alisema Obama katika taarifa yake.
"Mara kwa mara, nilimwona binafsi akiweka maslahi ya nchi yake mbele ya matamanio yake binafsi," aliongeza.
Obama alimsifu Odinga kwa ujasiri wake na utayari wa kufanikisha maridhiano ya amani "bila kuacha maadili yake ya msingi," akiongeza kuwa urithi wake utaendelea kusikika zaidi ya mipaka ya Kenya.
"Kupitia maisha yake, Raila Odinga aliweka mfano si kwa Wakenya tu, bali kote Afrika na duniani. Najua atakumbukwa sana," taarifa hiyo ilisema.
"Michelle na mimi tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia yake na kwa watu wa Kenya."
Obama amefanya ziara kadhaa zilizojulikana nchini Kenya, kwanza mwaka 2006 akiwa seneta wa Marekani kutoka Illinois, tena mwaka 2015 akiwa rais, na mara ya mwisho mwaka 2018 alipotembelea nyumbani kwa nyanya yake wa kambo, Sarah Obama, katika kijiji cha Kogelo, Kaunti ya Siaya.