Uturuki siku ya Jumatatu imelaani shambulizi la ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan na kuua walinda amani sita wa Bangladesh na kuwajeruhi wengine wanane.
"Tunawatakia rehema za Mwenyezi Mungu ziwafikie walinda amani wa Bangladesh waliopoteza maisha katika shambulio hili baya, na ahueni ya haraka kwa waliojeruhiwa," Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa.
Wizara hiyo ilisisitiza umuhimu wa kuhifadhi uhuru wa mipaka wa eneo la Sudan, na ikasisitiza "uungaji mkono mkubwa kwa juhudi zinazolenga kutafuta suluhu la amani kwa migogoro inayoendelea nchini humo."
Shambulio hilo limetokea huku mzozo kati ya jeshi la Sudan na kikosi RSF ukiendelea bila ya kusitishwa. Mapigano yalionaza tangu Aprili 2023 yamesababisha vifo vya maelfu, mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha moja ya machafuko mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Jeshi la Sudan lililaumu kikosi cha RSF. Hata hivyo hadi sasa hakuna ufafanuzi wowote kutoka kundi hilo la waasi.
Walinda amani hao walikuwa sehemu ya Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Abyei (UNISFA), kilichotumwa katika eneo la mpakani lenye mzozo la mafuta na linalosimamiwa na Sudan na taifa jirani la Sudan Kusini.
Wiki iliyopita, Sudan Kusini ilitangaza kuwa imefikia makubaliano ya pande tatu na jeshi la Sudan na RSF kuweka ulinzi katika uwanja wa mafuta wa Heglig-uliopo Kordofan Magharibi karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili-chini ya udhibiti wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF).
Makubaliano hayo yanaipa SSPDF "jukumu la msingi la kuweka usalama" katika mitambo ya mafuta huko Heglig.
Misheni ya ujumbe wa UNISFA liliongezwa mwezi uliopita.



















