Mgombea wa CCM Zanzibar: Hussein Ali Mwinyi
Mgombea wa CCM Zanzibar: Hussein Ali Mwinyi
Rais wa awamu ya 8 wa Zanzibar ni Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekuwa Rais wa visiwani huko tangu mwaka 2020 ikiwa ndiyo muhula wake wa kwanza.
12 Septemba 2025

Rais Hussein Ali Mwinyi yuko kwenye mchakato wa kuwaomba Wazanzibari wampe muhula mwingine kuwaongoza.

Dkt. Mwinyi ni mtoto wa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu Zanzibar na awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Ali Hassan Mwinyi.

 Dkt. Hussein Mwinyi alizaliwa Disemba 23, mwaka 1966. Masomo yake ya msingi na sekondari alisoma nchini Tanzania na katika taifa la Misri.

 Kitaaluma yeye ni daktari wa binaadamu ambapo alipata elimu hiyo katika Chuo Kikuu cha Marmara nchini Uturuki na baadaye kwenda nchini Uingereza alipopata shahada ya uzamili.

Amewahi kufanya kazi ya udaktari katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 Aliingia kwenye siasa mwaka 1999 na baadaye akateuliwa kuwa naibu waziri wa afya katika serikali ya awamu ya tatu.

 Mwaka 2005 alihamisha ngome yake ya kisiasa kutoka bara hadi visiwani na akapata ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka huo.

 Katika serikali ya awamu ya nne aliteuliwa kuwa waziri wa nchi na baadaye akawa waziri wa ulinzi.

 Pamoja na kuwa alirejea katika Wizara ya Afya kwa kipindi kifupi, amehudumu zaidi akiwa Waziri wa Ulinzi wa Tanzania.

Amekuwa pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

 Aligombea urais wa Zanzibar mwaka 2020 na akawashinda wagombea wengine 14 huku yeye akipata ushindi wa asilimia zaidi ya sabini.

Katika serikali yake amekuwa akiyapa kipaumbele masuala ya uwekezaji na kukabiliana na ufisadi.

Kwenye uchaguzi wa mwezi Oktoba, Dkt. Hussein Mwinyi ataminyana na wagombea kadhaa kutoka vyama vya upinzani.

 

CHANZO:TRT Afrika