| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ashiriki mazungumzo ya awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza
Mazungumzo hayo yalifuatia mikutano ya awali iliyofanyika Miami, Florida, nchini Marekani mwishoni mwa Disemba 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ashiriki mazungumzo ya awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza
Mkutano huo uliwaleta pamoja maafisa kutoka Marekani, Misri na Qatar kujadili maandalizi ya hatua inayofuata ya mpango wa amani wa Gaza. / / AA
12 Januari 2026

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, ameshiriki katika mkutano uliofanyika kupitia mtandaoni kilichojadili maandalizi ya awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza.

Kwa mujibu wa vyanzo vya wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, Fidan alijiunga na mkutano huo wa mtandaoni siku ya Jumatatu kama mwendelezo wa mazungumzo yaliyofanyika Miami, Florida, nchini Marekani mwishoni mwa Disemba 2025.

Mkutano huo uliwakutanisha maafisa kutoka Marekani, Misri na Qatar ili kujadili maandalizi ya hatua inayofuata ya mpango wa amani wa Gaza.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa Gaza tarehe 10 Oktoba chini ya mpango wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani Donald Trump, hatua iliyosimamisha mashambulizi ya Israel yaliyodumu kwa miaka miwili, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 70,000—hasa wanawake na watoto—na kujeruhi karibu watu 171,000 tangu Oktoba 2023.

Diplomasia

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki, Fidan pia alifanya mazungumzo ya simu kwa nyakati tofauti na mawaziri wa mambo ya nje wa Ugiriki na Uzbekistan.

Fidan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Giorgos Gerapetritis, walijadili uhusiano wa mataifa mawili pamoja na maendeleo ya kikanda.

Katika mazungumzo mengine ya simu, Fidan alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uzbekistan, Bakhtiyor Saidov. Wawili hao walijadili uhusiano wa mataifa mawili pamoja na masuala ya kikanda.

Pia walizungumzia maandalizi ya mkutano ujao wa Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.

Hakuna maelezo ya ziada kuhusu mazungumzo hayo yaliyotolewa.

CHANZO:AA