Ofisi ya Rais ya Uturuki imewasilisha rasmi pendekezo bungeni la kutaka kuongezwa kwa muda wa miezi 24 ya kikosi chake cha kijeshi nchini Libya, ikitaja kuendelea kutokuwa na uhakika wa kisiasa, changamoto za kiusalama ambazo hazijatatuliwa na haja ya kuhifadhi utulivu katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.
Hoja hiyo iliyotiwa saini na Rais Recep Tayyip Erdogan, iliwasilishwa kwa Bunge Kuu la Uturuki (TBMM) siku ya Jumapili. Ikiwa itaidhinishwa, mamlaka yataongezwa kutoka Januari 2, 2026, kwa miaka miwili zaidi.
Sababu za kupelekwa kwa jeshi la Uturuki
Hoja hiyo inakujua kufuatia juhudi za awali za kuanzisha taasisi za kidemokrasia nchini Libya kufuatia machafuko yaliyozuka mwaka 2011 zilidhoofishwa na kuongezeka kwa migogoro ya kivita, na kusababisha kugawanyika kwa muundo wa kisiasa na usalama.
Inaashiria Mkataba wa Kisiasa wa Libya, uliotiwa saini huko Skhirat, Morocco, mnamo Desemba 2015, ambao ulisababisha kuundwa kwa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa chini ya Azimio 2259 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kulingana na hoja hiyo, mashambulio yaliyoanzishwa mnamo Aprili 2019 yaliyolenga kuangusha serikali inayotambuliwa kimataifa yalisababisha Libya kuomba rasmi msaada kutoka Uturuki mnamo Disemba 2019.
Uturuki inasisitiza umuhimu wa amani na utulivu nchini Libya
Waraka huo unasema huku uwepo wa kijeshi wa Uturuki ulisaidia kusitisha mashambulizi na machafuko ya ndani, Libya bado hakuna usitishaji wa kudumu wa mapigano au kukamilisha mchakato wa mazungumzo ya kisiasa.
Inaonya kwamba kuendelea kutokuwa na uwezo wa kufanya uchaguzi kumeongeza hali ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa na changamoto za utawala, na kuweka hatarini utulivu uliopatikana na kuibua wasiwasi wa usalama kwa Libya na eneo zima.
"Kutokuwa na uwezo wa kufanya uchaguzi nchini Libya kumeongeza kutokuwa na uhakika wa kisiasa na matatizo ya utawala, na kuweka hatarini utulivu uliofanikishwa kwa kujitolea sana pamoja na kuweka tishio kubwa kwa utulivu wa kudumu," hoja hiyo ilisema.
Hoja hiyo inasisitiza kuwa kushindwa kuunganisha taasisi, hasa vyombo vya kijeshi na usalama, bado ni hatari kubwa kwa utulivu wa kudumu.
Jukumu la Uturuki na ushirikiano wa usalama
Hoja hiyo inasisitiza kwamba Uturuki inaendelea kutoa mafunzo na usaidizi wa ushauri kwa Libya chini ya Mkataba wa Maelewano wa Usalama na Kijeshi, ambao bado unatumika.
Inaongeza kuwa Ankara inachangia kikamilifu katika kudumisha utulivu, huku ikiunga mkono mazungumzo ya kijeshi na kisiasa yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yenye lengo la kuzuia kuzuka upya kwa mzozo.
Hati hiyo pia inasisitiza kwamba kurejea kwa mapigano kunaweza kuathiri vibaya maslahi ya Uturuki katika eneo la Mediterania na Afrika Kaskazini, huku ikiongeza hatari zinazohusiana na ugaidi, uhamiaji haramu na biashara haramu ya usafirishaji wa watu.
Muktadha wa kidiplomasia na kikanda
Uturuki inasalia kuwa mdau mkuu nchini Libya, ikidumisha ushirikiano wa kidiplomasia na usalama huku juhudi zikiendelea kuleta utulivu nchini humo.
Katika miezi ya hivi karibuni, mkuu wa ujasusi wa Uturuki Ibrahim Kalın alitembelea Libya kama sehemu ya mawasiliano yanayoendelea ya Ankara na wadau wa Libya. Uturuki pia imefanya juhudi za kuwasiliana na mkuu wa makundi yenye silaha mashariki mwa Libya Khalifa Haftar, akionyesha ushirikiano mpana na watendaji mbalimbali wa kisiasa na kijeshi huku kukiwa na mabadiliko ya mienendo nchini humo.
Ankara pia inaomba idhini ya bunge lenye makao yake mjini Tobruk nchini Libya, sambamba na Haftar, kwa makubaliano ya mamlaka ya baharini ya 2019 yaliyotiwa saini na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa huko Tripoli.
Mamlaka ya Bunge
Bunge la Uturuki liliidhinisha kwa mara ya kwanza kutumwa kwa wanajeshi nchini Libya mnamo Januari 2020, na muda huo uliongezwa mara kadhaa tangu hapo. Uidhinishaji wa sasa uliongezwa mara ya mwisho mnamo Novemba 2023.
Hoja ya hivi punde inataka idhini ya bunge kuongeza muda wa miezi 24, kulingana na Kifungu cha 92 cha Katiba cha Uturuki, kuruhusu serikali kujibu haraka kwa hatua zozote za kiusalama.



















