Spika wa Baraza la Wawakilishi la Australia, Milton Dick, ndiye atakayeongoza Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwa muhula unaofuata baada ya kushinda uchaguzi wa urais wa taasisi hiyo uliofanyika jijini Arusha, nchini Tanzania.
Dick amepata asilimia 56 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 9, wakati wa Mkutano wa 153 wa IPU katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Katika matokeo hayo, Spika wa Bunge la Azerbaijan Sahiba Gafarova amepata nafasi ya pili kwa asilimia 38 ya kura, huku Seneta wa Chile Robi Edwards akipata asilimia 6.
Ushindi huo unamaliza uongozi wa miaka mitatu wa aliyekuwa spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson wa Tanzania, ambaye amekuwa akiongoza taasisi hiyo inayoyaunganisha mabunge kutoka nchi mbalimbali duniani.
Akitoa ujumbe wake baada ya kutangazwa mshindi, Dick ameweka msisitizo katika mshikamano wa wabunge, akieleza kuwa tofauti za uchaguzi hazipaswi kuathiri ushirikiano ndani ya umoja huo.
“Leo hakuna mshindi wala mshindwa. IPU imezungumza kwa sauti moja. Hii ndiyo demokrasia,” amesema.
Amesisitiza kuwa viongozi wa mabunge wanapaswa kuendelea kusikilizana, kuheshimiana na kutumia mazungumzo kutafuta suluhu ya masuala yanayowakabili.
Dick amekuwa akiwakilisha jimbo la Oxley, Queensland, nchini Australia tangu mwaka 2016. Alichaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi mwaka 2022 na kupata muhula mwingine mwaka 2025 bila kupingwa.
Akiwa Rais wa IPU, anatarajiwa kusimamia mikutano rasmi ya Umoja huo na kuuwakilisha katika majukwaa makubwa ya kimataifa, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Anda Filip.
Mabadiliko hayo ya uongozi yanakuja wakati mabunge duniani yakiendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kujadili masuala ya demokrasia, uwakilishi wa wananchi na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi.
Mkutano wa 153 wa IPU unaoendelea Arusha ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya wabunge wa mataifa mbalimbali.
AFRIKA
2 dk kusoma
Milton Dick wa Australia aibuka rais mpya wa IPU, ahimiza umoja
Ushindi huo unamaliza uongozi wa miaka mitatu wa aliyekuwa spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson wa Tanzania, ambaye amekuwa akiongoza taasisi hiyo inayoyaunganisha mabunge kutoka nchi mbalimbali duniani.
Soma zaidi

















