Jeshi la Israel na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) zimekubaliana kuandaa mipango ya pamoja kwa ajili ya uwezekano wa kuongezeka kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, vyombo vya habari vya Israel viliripoti Jumamosi jioni.
Shirika la habari la Channel 13 la Israel limeripoti kuwa jeshi la Israel limethibitisha kuwepo kwa mipango hiyo ya pamoja na CENTCOM, huku likionya kuwa muda wa kufikia uamuzi kuhusu vita "unakaribia".
Hata hivyo, kwa mujibu wa shirika hilo, afisa mwandamizi wa Israel, ambaye hakutajwa jina, alisema kuwa suala la kufanya uamuzi wa kuishambulia Iran halikujadiliwa wakati wa ziara ya mkuu wa CENTCOM, Brad Cooper, mjini Tel Aviv.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa tathmini za kiusalama za Israel hazikuonyesha kuwa uwezekano wa kuanza tena kwa vita dhidi ya Iran ulikuwa mkubwa zaidi kuliko siku zilizotangulia.
Aidha, kiwango cha tahadhari katika jeshi la Israel kiliendelea kuwa juu, lakini bado hakijafikia kiwango chake cha juu kabisa, Shirika hilo habari limeongeza.
Kwa mujibu wa tathmini za jeshi la Israel zilizoripotiwa na kituo hicho, "wakati umefika kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kufanya uamuzi kuhusu kuchukua hatua dhidi ya Iran."
Ripoti hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa ya mvutano kufuatia mashambulizi ya kijeshi yaliyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28.
Iran ilijibu mashambulizi hayo kwa kuishambulia Israel pamoja na maeneo ambayo Iran ilieleza kuwa ni vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Ghuba.
Baadaye, Marekani na Iran zilitia saini hati ya makubaliano ya kuelewana (MoU) Juni 18 na kuanza mazungumzo. Hata hivyo, mazungumzo hayo hayakupiga hatua kubwa kutokana na kutokubaliana kuhusu masuala ya usafiri wa majini na usalama katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mapambano yalianza tena Julai licha ya juhudi za kidiplomasia zilizoendelea kufanyika kwa lengo la kumaliza mzozo huo.
Mkutano wa pande tatu wajikita katika utayari wa kijeshi
Jumatano, Brad Cooper alikutana na Mkuu wa Majeshi ya Israel, Eyal Zamir, pamoja na mkuu wa Shirika la Ujasusi la Mossad, Roman Gofman, mjini Tel Aviv. Mkutano huo ulifanyika wakati Israel ikiendelea kujiandaa kwa uwezekano wa kuanza tena kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Katika taarifa yake, jeshi la Israel lilisema kuwa Zamir na Cooper walifanya "tathmini ya pamoja na ya kina kuhusu hali ilivyo, na kujadili maendeleo ya kikanda pamoja na changamoto za kiusalama zinazowakabili kwa pamoja."
Taarifa hiyo iliongeza kuwa makamanda hao wawili pia walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kiutendaji kati ya majeshi hayo mawili, kuimarisha uratibu na kuongeza utayari wa pamoja wa kukabiliana na hali mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Hata hivyo, jeshi la Israel halikufafanua ni hali zipi hasa zilizojadiliwa wala kama mazungumzo hayo yalihusu moja kwa moja Iran.
Kwa upande mwingine, gazeti la Yedioth Ahronoth la Israel liliripoti Jumatano kuwa mkutano kati ya Cooper na Zamir ulijikita katika maandalizi ya kijeshi kwa uwezekano wa kuanza tena kwa vita dhidi ya Iran.
Mkutano huo ulifuatia ripoti zilizokuwa zikieleza kuhusu kuongezeka kwa maandalizi ya kijeshi ya Israel.
Novemba 11, shirika la utangazaji la Israel, KAN, liliripoti kuwa Baraza la Mawaziri la Usalama la nchi hiyo lilikuwa limeagiza jeshi kuongeza kiwango cha utayari kwa uwezekano wa kuishambulia Iran.
Mazungumzo ya kiintelijensia mjini Washington
Mkutano huo wa pande tatu ulifanyika siku chache baada ya mkuu wa Mossad, Roman Gofman, kutembelea Marekani kwa ajili ya kufanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa utawala wa Rais Donald Trump kuhusu Iran.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa Gofman alikutana na Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), John Ratcliffe, kujadili tathmini za kiintelijensia za Israel pamoja na uwezekano wa kuanzishwa tena kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran.
Wakati huohuo, viongozi wa kundi la kisiasa la upinzani la Israel linalojiita "kambi ya mabadiliko", linaloongozwa na Gadi Eisenkot, wamemtuhumu Waziri Mkuu wa mpito, Benjamin Netanyahu, kwa kusukuma ajenda ya kuanzisha vita vingine dhidi ya Iran.
Eisenkot, ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali ijayo ya Israel, pamoja na washirika wake, wanadai kuwa Netanyahu anataka kutangaza hali ya hatari nchini humo.
Kwa mujibu wa madai yao, hatua hiyo inaweza kulazimisha kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayomjumuisha Netanyahu na hivyo kumwezesha kuendelea kubaki madarakani.
Netanyahu anakabiliwa na kesi ya ufisadi ambayo, iwapo atapatikana na hatia, inaweza kusababisha kuhukumiwa kifungo cha gerezani.
Aidha, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetowa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu tangu mwaka 2024 kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza, zilizohusishwa na mashambulizi ya kijeshi ya Israel yaliyoanza Oktoba 2023.














