| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Waziri Mkuu wa Tanzania ataka Watanzania wapewe kipaumbele katika masuala ya ajira
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka wizara zinazohusika na masuala ya ajira kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa sheria zinazolinda nafasi za kazi kwa Watanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania ataka Watanzania wapewe kipaumbele katika masuala ya ajira
Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka wizara husika kusimamia kwa umakini usajili wa kampuni za kigeni. /Wengine / Others
14 Januari 2026

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa ajira zinazoweza kufanywa na wazawa hazipaswi kutwaliwa na wageni isipokuwa pale ambapo kuna uhaba wa utaalamu maalum nchini.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda maslahi ya wananchi na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Akizungumza Jumatano, Januari 14, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao cha mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za kisekta kilicholenga kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi, Dkt. Nchemba alisema mamlaka husika zina wajibu wa kusimamia sheria ipasavyo na kubaini mapungufu yoyote ya kisheria yanayoweza kuzuia utekelezaji wake. Alionya dhidi ya tabia ya kuruhusu wageni kufanya kazi ambazo Watanzania wana uwezo wa kuzifanya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekosoa mwenendo wa baadhi ya wamiliki wa nyumba kuwapangisha raia wa kigeni na kuwaruhusu kuwapangisha watu wengine wengi ndani ya makazi hayo, akieleza kuwa hali hiyo ni tishio kwa usalama wa taifa na pia inawakosesha Watanzania faida ya kiuchumi. Amehimiza Watanzania kuwa na uzalendo na “wivu wa nchi” kwa kulinda rasilimali na fursa zilizopo.

Dkt. Nchemba pia amezitaka wizara husika kusimamia kwa umakini usajili wa kampuni za kigeni, akibainisha kuwa baadhi ya taarifa zinazowasilishwa hazilingani na uhalisia.

Amesema sheria zilizopo zinalenga kukuza kampuni za Watanzania na kuhakikisha uwekezaji wa kigeni unazingatia maslahi ya taifa, huku akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wanaofuata sheria na kuchangia maendeleo endelevu ya nchi.

CHANZO:TRT Afrika