Akizungumza leo Januari 8, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya timu hiyo kutoka Morocco, Profesa Kabudi amesema wachezaji wameonesha ushindani, nidhamu na kujituma kwa kiwango cha juu, jambo lililoipa Tanzania heshima barani Afrika.
“Taifa Stars wameonesha umahiri wa hali ya juu na kujitoa kwa hali yao yote. Kwa mafanikio haya, Tanzania sasa si mshiriki tu wa AFCON, bali ni mshindani wa kweli,” amesema Profesa Kabudi.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni msingi mzuri wa maandalizi ya AFCON 2027 itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Aidha, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepanga kukutana na kikosi cha Taifa Stars Januari 10, 2026 kwa chakula cha mchana.
“Rais ameniagiza nije niwapokee na nimshukuru kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya michezo, ambao matunda yake yameanza kuonekana,” alisema.



















