Siku ya Jumanne jeshi la Benin limesema limewaua magaidi 45 katika kipindi cha miezi mitatu ya operesheni dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Benin.
Makundi yenye uhusiano na magaidi wa Al Qaeda huwa yanatishia usalama kaskazini mwa nchi.
2022, Benin ilipeleka takriban wanajeshi 3,000 kwa operesheni yake ya "Mirador" dhidi ya magaidi, na kwa sasa wameajiri wanajeshi wengine 5,000 kuimarisha usalama eneo la kaskazini.
Kati ya Oktoba na Disemba 2025, jeshi hilo "liliwakata makali magaidi 45 na kuwakamata washukiwa 7, ambao walifikishwa kwa mamlaka za mahakama", ulisema ujumbe wa jeshi ulioonekana na AFP.
'Kuwa makini bado ni muhimu'
Silaha, pikipiki, madumu ya petroli na magwanda ya jeshi yalipatikana "wakati wa makabiliano na adui ‘‘, Jeshi la Benin (FAB) lilisema, likipongeza "kuimarika" kwa uwezo wake.
"Shinikizo linalowekwa na FAB sasa linafanya iwe vigumu kwa makundi yenye silaha kuwepo kwa muda mrefu katika maeneo ya mpaka," jeshi lilisema.
Lakini liliongeza kwamba "kuwa makini bado ni muhimu."





















