Kupitia mkutano wao wa mtandaoni uliofanyika Machi 13, 2025, viongozi wa SADC wamekubaliana kuondoa majeshi yao ya kulinda amani ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“ Mkutano wa Marais umesitisha uwepo wa SAMIDRC na wameelekezwa kuanza kuondolowa kwa vikosi hivyo kutoka DRC,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya mkutano huo.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi, alikuwa ni mmoja ya viongozi waliohudhuria mkutano huo, akiwa pamoja na Marais wengine kutoka Zimbabwe, Botswana, Madagascar, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Tanzania na Zambia.
Novemba 2024, muda wa kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) chini ya mwamvuli wa SAMIDRC uliongezewa kwa mwaka mmoja na viongozi wa jumuiya hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweka wazi sababu za kuondoa vikosi hivyo ndani ya DRC.
Mashambulizi ya M23 yanayoendelea Mashariki mwa DRC yamesababisha wanajehsi wengi wa SAMIDRC kupoteza maisha wakiwa mstari wa mbele.
Wanajeshi wasiopungua 19 kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania waliuawa wakati M23 walipoteka mji muhimu wa Goma mwezi Januari.
Usalama wa kikosi cha SADC
Februari 2025, Malawi ilitangaza kuondoa majeshi kutoka kwa kikosi hicho.
Rais Lazarus Chakwera wa Malawi alisema kwamba uamuzi wake ulikusudia "kuheshimu tamko la kusimamisha mapigano ya pande zote."
Kulingana na Chakwera, hatua hiyo “itafungua njia ya mazungumzo yanayolenga kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo".
Katika shambulizi la Januari 2025, Afrika ilipoteza wanajeshi wake 14, hata hivyo nchi hiyo ikasema haitoondoa vikosi vyake.
" Kuwepo kwa majeshi ya Afrika Kusini nchini DRC kunategemea ujumbe wa SAMIDRC, ambao una muda wa kufanya kazi na tarehe ya mwisho kufanya hivyo,” alisema rais Ramaphosa alisema.
Nia ya kuleta amani
Ujumbe wa SADC ndani ya DRC ulitumwa Disemba 15, 2023 kuisaidia serikali ya nchi hiyo kurudisha amani na usalama mashariki mwa DRC.
Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC) kiko nchini DRC kusaidia serikali ya nchi hiyo kurejesha amani na usalama Mashariki mwa DRC.
Mnamo Mei 2023, SADC iliidhinisha SAMIDRC kuleta utulivu katika eneo hilo, na kuipa mamlaka ya kushiriki katika mapambano ya moja kwa moja na makundi yenye silaha.
Licha ya kuwa na idadi ya wanajeshi 5,000 kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania, ni wanajeshi 1,300 tu ambao wamepelekwa huko hadi kufikia sasa.
Eneo la Mashariki mwa DRC limeshuhudia ongezeko la migogoro na ukosefu wa utulivu wa utulivu na unaosababishwa na kuibuka kwa vikundi vyenye silaha.
DRC yakataa kikosi cha Afrika Mashariki
Viongozi wa Afrika Mashariki, ambayo ni sehemu ya DRC, walifanya uamuzi Julai 2022 wa kupeleka Kikosi cha Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mashariki mwa DRC . Hii ilikuwa baada ya ghasia mpya kutoka kwa kundi lenye silaha, M23.
Hata hivyo, ndani ya miezi 11, Rais wa DRC Felix Tshsiekedi hakuridhishwa na ufanisi wa kikosi cha kulinda amani cha EAC.
"Ujumbe uko wazi: Jeshi la kanda ya EAC ni lazima liondoke DRC ifikapo Disemba 8 kama ilivyokubaliwa, kwani imeshindwa kutatua tatizo, hasa lile la M23, " Waziri wa Mawasiliano wa DRC Patrick Muyaya alinukuliwa akisema.
Hapo ndipo jishi la SADC lilipopokea kijiti.
Likiwa limeundwa na wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania, kikosi cha SADC kilishirikiana na jeshi la ulinzi la DRC, maarufu kama FARDC, katika kupambana na makundi yenye silaha mashariki mwa DRC.
Uwepo wa SAMIDRC nchini DRC, ni kulingana na kanuni ya ulinzi wa pamoja na hatua za pamoja zilizoainishwa katika Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa SADC (2003).
Mkataba huo unasisitiza kuwa; "Shambulio lolote la silaha litakalofanywa dhidi ya moja ya Nchi Wanachama litachukuliwa kuwa tishio kwa amani na usalama wa kikanda na litakabiliwa na hatua za pamoja za haraka".
Nani atatoa usalama kwa DRC kwa sasa ?
Mkutano wa marais wa Afrika Kusini haujasema ikiwa kutakuwa na suluhisho mbadala wa kijeshi.
“ Mkutano wa marais ulisisitiza tena umuhimu wa suluhisho la kisiasa na kidiplomasia ambapo wadau wote katika mzozo nchini DRC wakiwemo wa kiserikali na sekta nyingine wa kijeshi na wasio wa kijeshi katika eneo la mashariki mwa DRC kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu nchini humo,” ulisema mkutano huo.
Uamuzi wa mkutano wa SADC sasa unafuta uamuzi wa mkutano wa pamoja wa SADC na Afrika Mashariki uliufanyika Februari 2025 kuamua kuwa wakuu wa majeshi wa nchi zao wakutane na kutafuta suluhu ya kudumu.













