| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
AU yakanusha tuhuma za Trump kuhusu mauaji ya halaiki Nigeria
Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai ya kwamba Wakristo wengi wanauawa nchini Nigeria, na hivyo kutishia kuwashambulia kundi la kigaidi linalotekeleza mauaji hayo.
AU yakanusha tuhuma za Trump kuhusu mauaji ya halaiki Nigeria
Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf amesema Waathirika wakuu wa Boko Haram ni Waislamu, si Wakristo. / / Reuters
13 Novemba 2025

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf amesema hakuna mauaji ya halaiki yanayoendelea kaskazini mwa Nigeria, akipinga madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyedai kuwa “idadi kubwa” ya Wakristo wanauawa katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.

“Kinachoendelea kaskazini mwa Nigeria si sawa na ukatili unaoshuhudiwa Sudan au katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema Mwenyekiti huyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa jijini New York.

“Fikiria kwanza kabla ya kutoa matamshi kama hayo,” aliongeza. “Waathirika wakuu wa Boko Haram ni Waislamu, si Wakristo.”

Kundi la kigaidi la Boko Haram, limekuwa likiendesha mashambulizi ya kikatili kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa zaidi ya miaka 15, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Wataalamu wa haki za binadamu wamesema waathirika wengi wa mashambulizi ya kundi hilo ni Waislamu.

Trump mapema mwezi huu alisema ameitaka Wizara ya Ulinzi kujiandaa kwa ajili ya uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi "haraka" ikiwa Nigeria itashindwa kukabiliana na mauaji ya Wakristo. Hakutoa ushahidi wowote maalum kwa ajili ya madai yake.

Pia alitishia "kusimamisha misaada yote na usaidizi kwa Nigeria, na huenda akaingia katika nchi hiyo ambayo sasa imefedheheshwa,' ili kuwaangamiza kabisa magaidi wanaofanya ukatili huu wa kutisha."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema nchi hiyo itaendelea kupambana na itikadi kali na kwamba inatumai Washington itaendelea kuwa mshirika wa karibu, ikisema "itaendelea kuwatetea raia wote, bila kujali rangi, imani au dini."

Nigeria, ambayo ina makabila 200 yenye itikadi ya Ukristo, Uislamu na dini za jadi, ina historia ndefu ya kuishi pamoja kwa amani.

Lakini pia imeshuhudia kuzuka kwa ghasia miongoni mwa vikundi, mara nyingi zikichochewa na migawanyiko ya kikabila au migogoro juu ya rasilimali.

CHANZO:Reuters