Mama Amina na harakati za kuokoa wenye matatizo ya afya ya akili Kenya
AFRIKA
6 dk kusoma
Mama Amina na harakati za kuokoa wenye matatizo ya afya ya akili KenyaKutoka umahiri wa masuala ya utalii hadi kuokoa maisha: Amina Abdallah, Mkurugenzi aliyeacha tasnia aliyopenda na kuamua kupambana na janga la afya ya akili.
Amina Abdallah, anayejitolea katika masuala ya afya ya akili / TRT Afrika Swahili
3 Desemba 2025

Takriban muongo mmoja uliopita, Amina Abdalla, kipindi hicho akiwa mmiliki wa kampuni ya utalii ya Tours and Safaris Limited, iliyokuwa na mafanikio mjini Mombasa, pwani ya Kenya, aliacha biashara hiyo, na yote yaliyompa fahari.

Kila kitu kilibadilika siku alipokutana na msichana mwenye umri wa takribani miaka ishirini, akitembea uchi mitaani huku watu wakimcheka. “Kama mzazi, sikuweza kupita tu,” Amina anakumbuka. Alimpeleka msichana huyo hospitalini na kugharamia matibabu yake ya afya ya akili kwa sababu, anavyosema, “Niliamini maisha yake yanaweza kuwa na matumaini.”

Kwa miezi sita, Amina alikuwa akimfuatilia msichana huyo ili aweze kupona. Alipomrudisha nyumbani, alimkuta baba yake ni kipofu, na maskini, na hakuwa na uwezo wa kumtunza. Miezi kadhaa baadaye, Amina alimpata msichana huyo akifanya biashara ya kuuza chapati na maharagwe, sasa akiwa ametulia kiakili na akimsaidia baba yake. “Kama ningemwacha vile nilivyompata, angeweza kudhulumiwa kingono, kupachikwa mimba au hata kupotea kabisa,” anasema Amina.

Tukio hilo lilibadilisha maisha yake. Aliuza magari yake ya biashara ya utalii, akijitolea kuwaokoa watu wanaoishi na matatizo ya afya ya akili mitaani. “Sikuona sababu ya kukaa ofisini nikisafirisha watalii. Niliamini ni wito wangu wa kufanya jambo ambalo Mungu angefurahia zaidi.”

Kabla kazi yake katika masuala ya afya ya akili haijafahamika kikamilifu, Amina tayari alikuwa ameanzisha shirika lisilokuwa la kiserikali la ‘‘Mombasa Women Empowerment Network’’ kama shirika la kijamii la kusaidia wanawake na watoto.

Lakini mahitaji makubwa aliyoyaona mitaani yalimfanya kupanua wigo wake. Alinunua ardhi, hata kabla ya kununua nyumba yake binafsi ya kuishi, na akajenga kituo cha kusaidia wenye matatizo ya afya ya akili. “Idadi ya wagonjwa ilikuwa kubwa mno, na gharama za matibabu zilikuwa juu. Nilijua nilihitaji kituo changu binafsi na daktari ili kupunguza gharama,” anaeleza.

Kila siku, Amina na wenzake huendesha gari wakipita mitaa ya Mombasa kuwaokoa watu. “Mara chache sana tunafika mjini kabla gari langu halijajaa,” anaiambia TRT Afrika. “Ukiwa pamoja na mimi, katika umbali wa chini ya kilomita moja naweza kuwakuta takriban watu kumi wagonjwa.” Huwa tunapokea simu hutoka viungani vya mji wa Mombasa na kaunti jirani.

Kilichoanza kama uokoaji wa muda sasa imekuwa kituo muhimu nchini Kenya kinachowaokoa watu wenye matatizo ya afya ya akili ambao hawajapata matibabu, kuwahudumia, kuwapa chakula, makazi, na elimu.

Kwa Amina, mitaa imekuwa wito wake kwa sababu ameona kwa macho yake unyama wanaopitia wagonjwa wa akili. Wengi hutengwa, kudharauliwa, au huitwa majina ya kejeli kama “wendawazimu,” “wamerogwa,” au “wamekabiliwa na mapepo.” “Hawatendewi haki kama binadamu wengine,” anaeleza. “Na unapomtendea mtu hivyo, anaanza kuamini kuwa yeye si wa dunia hii.”


Imani za kitamaduni husababisha kuwepo kwa changamoto kubwa zaidi. “Afya ya akili sio kile watu wanachofikiria,” Amina anasema. “Familia nyingi hushindwa kwa sababu wanaamini ni uchawi au laana.” Mtu anapojizungumzisha peke yake, familia hudhani ni mapepo. Katika familia nyingi, tabia zisizo za kawaida huhusishwa na adhabu kutoka kwa Mungu au laana.

Kufikiria hivyo hufanya familia kukataa kabisa matibabu ya kitaalamu. “Kwa miaka mingi, watu waliamini huwezi kupona,” anasema. “Waliwaita walioathirika waliolaaniwa, wamerogwa, au kuwatenga.”


Lakini unyanyapaa unazidi utamaduni. Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya ya akili. Mombasa, jiji lenye zaidi ya watu milioni moja, lina chini ya matabibu wa magonjwa ya akili kumi pekee.

Kwa kuwa matatizo ya akili yanaathiri mtu mmoja kati ya wanne, mfumo hauwezi kukabiliana. “Wagonjwa wengi hawatibiwi, hawaonekani, hawasikiki,” Amina anasema.

Msaada wa serikali ni mdogo, na upatikanaji wa vifaa vya kufanya vipimo vya kama ubongo vinavyotumika nchi nyingine bado haupatikani. Matibabu yanategemea vipimo vya kitaalamu na dawa pekee, na kuifanya Kenya kubaki nyuma ikilinganisha na viwango vya kimataifa.

Kuwepo kwa mwanya huu, kazi ya Amina imekuwa msaada muhimu. “Tangu wakati huo, nimejitolea kuwasaidia watu wenye matatizo ya akili, hasa wanaoishi mitaani,” amesema.

“Kwa kipindi hiki kirefu, nimewaokoa zaidi ya wagonjwa 2,000.” Wengi wakiwemo waliotembea kutoka Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hata Uingereza. Matatizo ya akili mara nyingi humfanya mtu kutembea umbali mrefu bila kujielewa anakotoka au anakokwenda.

Kubadilisha mitazamo ya jamii imekuwa sehemu muhimu ya dhamira yake. Huwa na ujumbe wa huruma kwa njia rahisi na zenye uhalisia. “Ukiwaona, hata kama wanaonekana wanatia hofu, wape maziwa, wape mkate, usiwakimbie,” anahimiza. Muenendo wake unazingatia utu. Watu wanapoona wagonjwa wakipona, wanaanza kuelewa kuwa afya ya akili ni ugonjwa wa kawaida unaoweza kutibiwa.

Tuzo halisi kwa Amina iko katika mabadiliko. “Hakuna kinachonipa furaha kuliko kumchukua mtu aliyepotea mitaani, kumtibu, na kumwona akipona,” anasema. Anakumbuka kuona wagonjwa wa zamani wakirudi katika maisha yao ya ibada, kurudi kwa familia zao, na kufanya kazi tena.

Baadhi sasa ni madereva wa malori ya kusafirisha mizigo Afrika Mashariki. “Niliwachukua kutoka mitaani. Hizi ni simulizi za mafanikio ndizo zinazonipa nguvu kila siku.”

Kazi yake ya kujitolea imetambuliwa. Mama Amina ametunukiwa tuzo za kitaifa na kimataifa kwa mchango wake, ikiwemo Tuzo ya Mashujaa Day (Shujaa wa Taifa) mwaka 2021, Tuzo ya Good Citizen ya Rotary Club of Mombasa, kutambuliwa miongoni mwa Waislamu 100 Wenye Ushawishi Zaidi Kenya, na pia katika Wanawake 50 Wenye Ushawishi Zaidi Kenya. Tuzo hizi zinaonesha si tu huduma yake, bali pia maisha aliyowarejesha watu na namna anavyokabiliana na changamoto katika huduma ya afya ya akili.

Lakini pia anaona sababu kuu katika matukio haya ya matatizo ya akili: umaskini. “Umaskini unachangia sana katika matatizo ya afya ya akili,” amesema. Watu wengi huishia kuwa na msongo wa mawazo kutokana na ukosefu wa kazi, makazi, na shinikizo kutoka kwa jamii. Mihadarati na utafunaji rahisi kama mogoka huongeza tatizo. Kwa familia maskini, matibabu hayalipiki. “Zaidi ya asilimia 80 ya watu ninaowaokoa wanatoka katika mazingira duni,” anasema. Hizi ni familia ambazo hazina hata uhakika wa mlo wa siku. Anawasaidia kwa kuwapa dawa bila malipo na mafunzo ya ujuzi, akilenga kuwaondoa “kutoka mitaani hadi kujitegemea.”

Kuendesha kituo kuna changamoto ya kifedha. Gharama za chakula hufikia shilingi milioni 1.1 za Kenya kwa mwezi, na wafadhili hujaza pengo hilo kwa sehemu ndogo tu. Dawa zinahitaji shilingi za Kenya 650,000 zaidi. Bila wafadhili rasmi, kituo kinaishi kwa moyo wa kujitolea na juhudi za Amina na familia yake.

Hata hivyo, baada ya miaka ya kuwaokoa watu ambao jamii imewasahau, Amina anaamini huruma pekee haitoshi. “Ili kuleta mabadiliko ya kweli, ninahitaji kuingia uongozini,” amesema.

Anahoji kuwa licha ya Katiba ya Kenya kulinda haki za watu wenye matatizo ya akili, lakini bila utekelezaji, hakuna mabadiliko ya hali yao. “Haki zao zipo kwenye karatasi tu, lakini si kwenye maisha. Nani atapigania haki zao kama si mtu kama mimi anayehisi uchungu wao usiku na mchana?”

Anaona mustakabali ambapo kila kaunti nchini Kenya, na kila nchi Afrika, ina vituo vya uokoaji, huduma za ukarabati, upatikanaji wa dawa, na miradi ya kuwarejesha tena katika jamii. “Watu wenye saratani, VVU, au Kifua kikuu hupatiwa huduma hadi majumbani mwao,” anasema. “Lakini wagonjwa wenye matatizo ya akili, ambao ni dhaifu zaidi, huachwa nje kama wanyama.”

Kwa Amina Abdalla, kuingia kwenye uongozi si tamaa. Ni wajibu. Safari yake ilianza kwa kumuokoa msichana mmoja. Leo, yuko tayari kupigania maelfu zaidi, akiwa na azma ya kuwatetea kwa kile ambacho jamii imewanyima kwa muda mrefu: hadhi, ulinzi, na mahali pa kustahili.