Lesotho inajivunia ishara yake ya kitaifa kupitia kofia inayoitwa Mokorotlo.
Huu ni utambulisho wa watu wa taifa lililoko Kusini mwa Afrika.
Lesotho ni nchi ndogo iliyozungukwa kabisa na Afrika Kusini, lakini imetenganishwa na milima.Watu wa Lesotho, ambao ni zaidi ya milioni mbili, wanaendeleza baadhi ya mila na lugha zinazofanana na watu wa Afrika Kusini.
Lugha yao, Sesotho, pia ni mojawapo ya lugha 11 rasmi za Afrika Kusini. Kwa
hakika, watu wengi zaidi wanaizungumza nchini Afrika Kusini - milioni 4.6 -
kuliko Lesotho.
Lesotho iliyopata uhuru wake kutoka Uingereza 1966, ina utawala wa kifalme, huku Mfalme Letsie wa tatu akiwa kiongozi rasmi wa nchi, Kiongozi wa serikali ni Waziri Mkuu.
Kuna bunge la Seneti lenye wajumbe 33 na Bunge la Kitaifa linalowakilishwa na wabunge 120.Kofia hii Mokorotlo ni ishara ya umoja wao.
Kofia hii imetengenezwa kutoka kwa nyasi asilia inayojulikana kama "mosea"
au "leholi".
Muundo wake unaaminika kuwa ulichochewa na huu mlima
uitwao Qiloane uliopo nchini humo.Kofia pia inajulikana kama "molianyeoe",
ikiwa na maana ya "anayetekeleza hukumu mahakamani" kwa lugha ya Sesotho.
Picha yake inaonekana kwenye bendera ya Lesotho, na kwenye nambari za usajili za magari ya nchi hiyo.Wasotho hupamba majumba na kofia za mokorotlo, ishara
ya kuendeleza mila.
Pia inaaminika kuilinda nyumba dhidi ya hatari na mambo mengine mabaya.Kofia hii ni sehemu muhimu ya mavazi ya kitamaduni ya Wasotho ambayo huvaliwa kuonesha utambulisho wao na fahari ya kitaifa.Ingawa kwa kawaida hunasibishwa na wanaume,
wanawake na watoto pia huvaa kofia hiyo pia.
Mokorotlo mara nyingi hutumika katika sherehe za kitamaduni, kama vile harusi na tambiko,Licha ya mitindo ya kisasa kuingia katika jamii, umuhimu wa kofia ya mokorotlo unaendelea kustawi, ukionesha uthabiti na fahari ya utamaduni wa Basotho katika jamii ya kisasa.
Ubunifu wa kutengeneza mokorotlo unarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ikidhihirisha ustadi wa mafundi wanaoitengeneza.













