| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Korea Kusini, India zataka raia wake kuondoka Iran kufuatia hofu ya mashambulizi ya Marekani
Korea Kusini inasisitiza kwamba wale wanaopanga kusafiri Iran wasitishe mipango ya safari zao kwa muda au waahirishe.
Korea Kusini, India zataka raia wake kuondoka Iran  kufuatia hofu ya mashambulizi ya Marekani
Korea Kusini inasisitiza kwamba wale wanaopanga kusafiri Iran wasitishe mipango ya safari zao kwa muda au moja kwa moja. / AP
23 Februari 2026

Korea Kusini na India zimewatahadharisha raia wake kuondoka Iran wakati hali ya wasiwasi ikiongezeka kufuatia uwezekano wa taifa hilo kushambuliwa na Marekani, hii ni kwa mujibu wa taarifa za balozi.

Katika taarifa yake ya usalama kupitia mtandaoni, Ubalozi wa Korea Kusini nchini Iran umeonya kwamba hali ya usalama ya nchi hiyo inaweza kusambaratika ghafla. Hivyo imewataka raia wa Korea Kusini kufuatilia kwa karibu taarifa za vyombo vya habari na ushauri unaotolewa na ubalozi, na kuchukua tahadhari ya ziada ili kuhakikisha usalama wao.

“Taarifa za habari za hivi karibuni zimeonesha kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika eneo hilo, na kutaja uwezekano wa Marekani kuishambulia Iran huku Iran ikitahadharisha kulipiza," kwa mujibu wa ubalozi.

Ubalozi umewashauri raia wa Korea Kusini ambao hivi sasa wapo nchini Iran kuondoka nchini humo "haraka iwezekanavyo" isipokuwa kwa wenye dharura ya kubaki.

Pia imewakata wenye mpango wa kwenda Iran kusitisha mpango huo kwa muda au kuahirisha.

Katika taarifa tofauti kupitia mtandao wa X, Ubalozi wa India jijini Tehran umewashauri raia wake kuondoka nchini Iran kwa kutumia njia yoyote inayowezekana, ikiwemo ndege za abiria.

Ubalozi huo pia umewataka raia wake kuwasiliana na ubalozi iwapo watahitaji msaada wowote na kuweka namba za mawasiliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Serbia nae amewataka raia wake kuondoka nchini Iran "haraka iwezekanavyo" na kuwashauri dhidi ya kusafiri, kwa madai ya kudorora kwa hali ya usalama iliyohusishwa na hali ya wasi wasi iliyopo katika eneo hilo, imeripoti Gulf News.

Tahadhari hii inatolewa wakati ambapo Marekani imeongeza uwepo wake wa kijeshi Mashariki ya Kati.

Rais wa Marekani Donald Trump Alhamisi iliyopita ametoa muda wa siku 10- hadi 15-za mazungumzo na Iran kabla ya kufikiria kutumia nguvu za kijeshi.