Rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, ameshtakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ambapo anadaiwa kushiriki katika mauaji ya watu karibia 76 wakati wa kampeni yake ya “vita dhidi ya madawa ya kulevya”.
Mashtaka dhidi ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 80, ambaye amekuwa gerezani nchini Uholanzi tangu mwezi Machi, yamewekwa wazi kwenye waraka uliochapishwa na ICC Jumatatu.
Mashtaka hayo pia yanahusiha sehemu moja ya kampeni kali ya kupambana na madawa ya kulevya iliyoongozwa na Duterte alipokuwa rais, ambayo ilisababisha vifo vya maelfu ya watu waliodaiwa kuwa wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Kulingana na waraka ya mashtaka wa ICC na kusainiwa na msaidizi wa mashtaka wa mahakama hiyo, Mame Mandiaye Niang, wakili wa mashtaka anaona kuwa Duterte ni mhusika wa moja kwa moja katika mauaji yaliyotokea kati ya mwaka 2013 na 2018.
Kesi ya kwanza inahusiana na kipindi chake akiwa Meya wa Jiji la Davao, ambapo anadaiwa kuwa “mhusika asiye wa moja kwa moja” katika mauaji 19 kati ya 2013 na 2016.
Mashtaka ya pili na ya tatu yanahusu miaka yake akiwa rais. Aidha kesi ya pili inahusu mauaji ya walengwa 14 waliodaiwa kuwa na umuhimu mkubwa kati ya 2016 na 2017, huku kesi ya tatu ikihusu mauaji 43 yaliyofanywa wakati wa operesheni za ‘kuondoa’ dhidi ya wahalifu wa ngazi ya chini kati ya 2016 na 2018.
Kati ya mauaji hayo 76 yalitekelezwa na polisi kwa mujibu wa ICC.
Hata hivyo mahakama inapaswa kwanza kuamua kama rais huyo wa zamani yuko katika hali nzuri ya kisheria kuweza kushtakiwa, baada ya wakili wake, Nicholas Kaufman, kupendekeza kesi hiyo ichelweshwe kwa muda usiojulikana kutokana na hali mbaya ya afya ya Duterte.
Kaufman amesema Duterte anakumbwa na ugonjwa wa “kupoteza fahamu”.
Duterte alikamatwa jijini Manila, mji mkuu wa Ufilipino, tarehe 11 Machi, na haraka akapelekwa Uholanzi ambapo amekuwa gerezani chini ya ICC. Duterte anasisitiza kuwa kukamatwa kwake ni kinyume cha sheria.
Wafuasi wa Duterte nchini Ufilipino wanasema kuwa kukamatwa kwake ni siasa na ni matokeo ya mzozo kati ya familia yake na rais wa sasa wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr.