Waasi wanaomiliki kibali cha dhahabu cha kampuni ya Twangiza Mining mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamepora takriban kilo 500 za dhahabu tangu Mei, kampuni hiyo iliiambia Reuters, ikiwashutumu baadhi ya wafanyakazi wake kwa kusaidia wizi huo.
Kwa bei za sasa, dhahabu iliyoporwa ina thamani ya karibu dola milioni 70.
Mgodi huo uko katika eneo la Kivu Kusini, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda walifanya mashambulizi makali mwaka huu na kuwaruhusu kuteka maeneo mengi zaidi kuliko hapo awali. Waliuteka mgodi huo mwezi Mei.
"Kwa msaada wa baadhi ya wafanyakazi, walisafirisha shehena ya kwanza ya zaidi ya kilo 50 za dhahabu nje kwa muda mfupi sana," Twangiza Mining ilisema Jumatatu katika majibu ya maandishi kwa maswali ya Reuters kuhusu hasara tangu M23 kudhibiti mgodi huo.
"Tangu kazi hiyo, wamepata angalau kilo 500 za dhahabu na kuzisafirisha kwa siri kupitia njia za chini ya ardhi," kampuni hiyo ilisema.
Shirika la Reuters linasema M23 haikujibu mara moja ombi la maoni.
Kampuni ya uchimbaji madini ya Twangiza ambayo ina makao yake makuu nchini DRC na inajieleza kuwa ni kampuni ya China, imesema ilipoteza zaidi ya kilo 100 za dhahabu kwa mwezi tangu kuchukuliwa, pamoja na vifaa vya thamani vya dola milioni 5.
Kampuni hiyo inajiandaa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa usuluhishi wa kimataifa na mamlaka za Congo, ilisema.
Iliwashutumu waasi hao kwa kuwafukuza wakazi, kubomoa makanisa na kutumia mafundi wa Rwanda kuchukuwa data za kijiolojia ili kuanza tena na kupanua uchimbaji madini. "Kuna zaidi ya wafanyakazi 150 waliosalia’’.
Hatuwezi kuwasiliana nao," kampuni hiyo ilisema. Serikali ya Rwanda haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mnamo Oktoba 15 yaliharibu miundombinu ya kuzalisha umeme kwenye mgodi huo.
Haijabainika ni nani alihusika na shambulio hilo la ndege zisizo na rubani. Mapigano mashariki mwa Congo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya maelfu wengine kuyahama makazi yao mwaka huu.
Makundi yenye silaha yameteka maeneo kadhaa ya uchimbaji madini mashariki mwa DRC yenye utajiri mkubwa wa madini, kulingana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka jana lilisema waasi wa M23 walikuwa wakipata karibu dola 300,000 kila mwezi kutokana na ushuru wa madini katika eneo lenye utajiri wa madini ya coltan, Rubaya.
Rais wa Marekani Donald Trump aliafiki makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda mwezi Juni kama sehemu ya juhudi za kuleta utulivu mashariki mwa Congo na kuleta uwekezaji wa madini kutoka mataifa ya Magharibi.
Rwanda imekuwa ikikanusha kuwaunga mkono waasi wa M23, licha ya madai ya mara kwa mara kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa na serikali za kikanda.
Qatar imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya DRC na M23.
Pande hizo mbili zilikosa kufikia muafaka kufikia muda wa mwisho wa kufanya hivyo Agosti, ikiwa ni makubaliano ya amani kama sehemu ya mchakato huo lakini mnamo Oktoba 14, walikubaliana na utaratibu wa ufuatiliaji wa kusitishwa kwa mapigano.