| Swahili
MICHEZO
2 dk kusoma
Misri si miongoni mwa timu zinazotarajiwa kushinda AFCON, anasema Salah
Mshambuliaji wa Misri Mohamed Salah amesema timu yake haipo miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kushinda Kombe la AFCON, lakini amesisitiza kuwa watapambana kwa nguvu zote ili kufika hatua za juu zaidi za mashindano hayo yanayofanika Morocco.
Misri si miongoni mwa timu zinazotarajiwa kushinda AFCON, anasema Salah
Mohamed Salah alisema hakuna mechi rahisi katika AFCON. / / Reuters
6 Januari 2026

Salah, ambaye ni mshambuliaji wa Liverpool, alifunga bao la tatu na kuihakikishia Misri nafasi ya kufuzu robo fainali baada ya ushindi mgumu dhidi ya Benin siku ya Jumatatu.

Mechi hiyo iliisha kwa mabao 3-1 baada ya kuongezwa kwa muda wa ziada.

Timu ya kocha Hossam Hassan inalenga kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, na kwa jumla mara ya nane, katika mashindano hayo.

“Sidhani kama sisi ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kushinfa AFCON,” Salah aliwaambia waandishi wa habari.

“Tuna wachezaji vijana, na wengi wao wanacheza ndani ya Misri. Tunapigania taifa letu tu… kila mtu anatoa mchango wake wote, na mmeona hilo leo.”

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema hakuna mechi rahisi katika AFCON.

“Viwango vya timu vinakaribiana; niliwaambia wenzangu jana kuwa hakuna timu inayofungwa mabao manne au matano. (Benin) wana timu nzuri na kocha mzuri… ninafurahi kwamba hatimaye tuliweza kushinda.”

Salah amefunga mabao 10 katika mechi 22 za AFCON, akihitaji mabao mawili kufikia rekodi ya Hassan El-Shazly ambaye ni mfungaji bora wa timu hiyo katika mashindano hayo, huku akihitaji bao bao moja kumfikia kocha wake wa sasa, Hassan.

Misri itakutana na mabingwa watetezi Ivory Coast au Burkina Faso katika robo fainali itakayochezwa Agadir, Morocco siku ya Jumamosi.

CHANZO:Reuters