| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Eritrea inakana kutuma shehena ya risasi nchini Ethiopia
Polisi nchini Ethiopia wamesema wamekamata zaidi ya risasi 56,000, ambazo Ethiopia inadai zilitumwa kutoka nchi jirani ya Eritrea.
Eritrea inakana kutuma shehena ya risasi nchini Ethiopia
Ethiopia inadai kuwa zaidi ya risasi 56,000 zimetoka Eritrea, madai ambayo Eritrea inayakanusha. /AP / AFP
tokea masaa 12

Katika taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wao wa Facebook siku ya Jumatano, polisi nchini Ethiopia walisema walikamata “zaidi ya risasi 56,000” katika eneo la Amhara, ambazo zilikuwa zimekusudiwa “kutumwa” kwa kundi la waasi ndani ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa polisi wa Ethiopia, risasi hizo zilisafirishwa kwa lori kutoka Eritrea na kupitishwa kupitia eneo la kaskazini la Tigray kwa msaada wa Kundi la Tigray la (TPLF).

Eritrea yakana shutuma za Ethiopia

Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Ghebremeskel, aliliambia shirika la AFP kwamba Ethiopia “inatoa taarifa za uongo.”

TPLF pia ilikana tuhuma hizo na kuzitaja kuwa “zisizo na msingi.”

Eritrea ilipata uhuru wake kutoka Ethiopia mwaka 1993. Nchi hizo mbili zilipigana vita vya mpakani kuanzia 1998 hadi 2000.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed awali alitaka kuimarisha uhusiano na Eritrea alipoingia madarakani, jambo lililompatia Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019.

Mivutano

Serikali za nchi hizo mbili zilishirikiana kupambana na makundi yenye silaha ya Tigray wakati wa vita vya miaka 2020 hadi 2022, lakini baadaye ziligombana kufuatia makubaliano ya amani ambayo Eritrea haikuhusishwa.

Katika miezi ya hivi karibuni, uhusiano wao umezidi kuzorota.

Katika mahojiano na runinga ya taifa siku ya Jumatatu, Rais wa Eritrea Isaias Afwerki alielezea hatua za Ethiopia kuwa zinachochea mvutano.

Ethiopia ilidai mwezi Oktoba 2025 kwamba Eritrea ilikuwa ikijaribu kuisambaratisha kwa kuunga mkono makundi yenye silaha, hasa katika eneo la Amhara. Eritrea ilisema madai hayo si “ya kweli.”

CHANZO:AFP