Profesa Phoebe Okowa wa Kenya amechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), na kuashiria hatua nyingine muhimu kwa taifa hilo katika ngazi za Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Kenya Korir Sing’oei, aliupongeza uchaguzi huo kama ishara ya utaalamu wa kisheria wa Okowa na kuheshimiwa kwa Kenya katika masuala ya kimataifa.
"Mafanikio haya yanaonyesha imani katika uwezo wa Okowa kwenye mahakama na hadhi ya Kenya," Sing'oei alisema katika mtandao wa X muda mfupi baada ya tangazo hilo.
"Ninapongeza maafisa wa New York na Geneva kwa kuongoza na kuhakikisha sauti ya Kenya inaendelea kusikika katika majukwaa ya mahakama ya kimataifa, "aliongeza.
Okowa, ambaye kwa sasa anahudumu kama mjumbe wa Tume ya Kimataifa ya Sheria, alichaguliwa Jumatano jioni baada ya kinyang'anyiro kikali katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).
Msomi huyo aliyebobea katika masuala ya sheria za kimataifa alipata wingi wa kura zinazohitajika katika duru ya nne ya upigaji kura UNGA na duru ya tatu katika Baraza la Usalama, akiwashinda wagombea wengine watatu waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ili kumrithi Jaji wa Somalia Abdulqawi Ahmed Yusuf.
Kujiuzulu kwa Jaji Yusuf, kuanzia Septemba 30, 2025, kulitoa nafasia kwa jopo hilo la majaji 15 wa ICJ, ambayo iko The Hague, Uholanzi.
Okowa alipata kura 106 kati ya 185 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na kupita kiwango cha kura 97 na alipata kura nane kati ya 15 za Baraza la Usalama, idadi ya chini inayohitajika ili kuchukua nafasi hiyo.
Aliteuliwa kwa pamoja na Colombia, Kenya, Namibia, Uholanzi, Romania, Afrika Kusini, Sweden, na Vanuatu. Atakuwepo kwenye nafasi hiyo hadi Februari 5, 2027, muda uliosalia wa kipindi cha Jaji Yusuf.
Okowa anakuwa Mkenya wa kwanza kuhudumu kama jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, na hivyo kuashiria hatua ya kihistoria kwa taifa hilo na kanda.
Sasa anajiunga na jopo lililochaguliwa la wanasheria wa Kiafrika ambao wamehudumu katika Mahakama, akiwemo Abdul Koroma wa Sierra Leone na Abdulqawi wa Somalia.
Uchaguzi wake unaimarisha zaidi uwakilishi wa Kenya katika vyombo vya juu vya sheria vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Tume ya Kimataifa ya Sheria, ambako amehudumu pia.













