Wabunge wa nchini Marekani wanatarajiwa kuitembelea Tanzania mwakani, kufuatia mwaliko rasmi kutoka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mwaliko huo, unafuatia majadiliano yaliyojiri kati ya Kombo na mjumbe wa Bunge la Marekani na kamati ndogo ya bara la Afrika, Ronny L. Jackson.
Kulingana na taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa wa X wa Wizara hiyo Disemba 17, 2025, wawili hao walijadiliana masuala mbalimbali ikiwemo ziara ya wabunge hao nchini Tanzania mwakani.
Kikao hicho pia kilitoa fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu maslahi ya pande zote mbili, ikiwemo ushirikiano wa kidiplomasia, masuala ya kikanda na kimataifa pamoja na maeneo ya kuongeza ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Hali kadhalika, wakati wa majadiliano hayo, Jackson alirejelea ziara ya awali aliyoifanya nchini Tanzania, akioneshwa kuvutiwa na ukarimu wa Watanzania na urithi na utajiri wa kitamaduni wa nchi hiyo.
Mwaliko huo unakuja wiki chache, baada ya serikali ya Marekani kusema kuwa inatathimini upya uhusiano wake na Tanzania.

















