Uturuki na Urusi zimethibitisha tena dhamira yao ya kuongeza biashara ya pande mbili na kufikia Dola bilioni 100 kwa mwaka, ikiwa ni mara mbili ya kiwango cha sasa.
Waziri wa Biashara wa Uturuki, Omer Bolat, na Naibu Waziri Mkuu wa Urusi, Alexander Novak, walisaini tamko la pamoja mjini Istanbul siku ya Ijumaa, baada ya kukamilika kwa mkutano wa 20 wa Tume ya Biashara na Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Urusi na Uturuki.
Bolat alisema kuwa biashara ya kila mwaka kati ya nchi hizo mbili kwa sasa inafikia Dola bilioni 50, na kwamba pande zote mbili zinalenga kuongeza kiwango hicho hadi Dola bilioni 100. Aliongeza kuwa mazungumzo yao yalihusu biashara, usafirishaji, nishati na utalii.
Kwa upande wake, Novak alisema kuwa Uturuki ilikuwa mshirika wa pili kwa ukubwa wa biashara wa Urusi mwaka 2025, lakini ilishika nafasi ya nne katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2026.
Alieleza kuwa biashara ya bidhaa za kilimo na zinazohusiana na sekta hiyo iliongezeka kwa asilimia 12 katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2026, huku mauzo ya bidhaa hizo kutoka Urusi kwenda Uturuki yakiongezeka kwa asilimia 17. Aliongeza kuwa Uturuki iliendelea kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa nafaka kutoka Urusi.
Novak pia alizungumzia uzinduzi wa kiwanda cha kwanza cha Uturuki cha kuzalisha kemikali au kaboni inayotumika katika utengenezaji wa resini, mipako, plastiki, na dawa, uliofanyika siku ya Alhamisi katika eneo la viwanda la GEBKIM, mkoani Kocaeli.
Alisema kiwanda hicho kitawawezesha wazalishaji wa Uturuki wanaotengeneza rangi, vanishi na vifaa vya ujenzi kupata kemikali hiyo ndani ya nchi, badala ya kutegemea vyanzo vya nje.
“Uturuki na Urusi, ambazo ni nchi jirani, zenye urafiki na washirika muhimu wa kibiashara, zitaendelea kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi kwa kasi zaidi hadi mwaka 2027,” alisema Novak.
Ushirikiano katika sekta ya nishati na utalii
Novak alisema kuwa Urusi inaendelea kuizuia Uturuki gesi asilia, na mafuta ghafi. Alibainisha kuwa usafirishaji wa gesi asilia unaendelea bila kukatizwa kupitia mabomba ya Blue Stream na TurkStream.
Kuhusu mradi wa Kiwanda cha Kuzalisha Umeme wa Nyuklia cha Akkuyu, alisema kuwa kazi zinaendelea katika mitambo yote minne ya mradi huo, huku maandalizi yakielekezwa katika kuhakikisha mtambo wa kwanza unaanza kufanya kazi.
Katika sekta ya utalii na usafirishaji, Novak alisema kuwa mashirika ya ndege ya Urusi yaliwasafirisha zaidi ya abiria milioni 6.5 kati ya nchi hizo mbili mwaka uliopita. Wakati huohuo, karibu watalii milioni saba kutoka Urusi walitembelea Uturuki, na hivyo kuifanya Urusi kuwa nchi inayoongoza kwa idadi ya watalii wanaotembelea Uturuki.
Aidha, Novak alibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo katika sekta za afya, utengenezaji wa dawa, teknolojia za kidijitali, huduma za ugavi na biashara za mtandaoni.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika nyanja za elimu, michezo na tamaduni kati ya mataifa hayo mawili.














