Wachezaji saba wa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Iran, wamepewa hifadhi ya kisiasa nchini Australia baada ya kugoma kuimba wimbo wa taifa katika mchezo wa Kombe la Asia, mwishoni mwa juma.
Hata hivyo, mmoja kati ya wachezaji hao, alibadili maamuzi yake, na kuomba kurudi nchini Iran, kulingana na Shirika la Habari la Australia.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia Tony Burke alithibitisha taarifa hizo, akisema kuwa mchezaji huyo aliwasiliana na maofisa katika ubalozi wa Iran, ambao walikuja kumchukua katika hoteli aliyofikia na wenzake ambao wameamua kubakia Australia.
Kulingana na waziri huyo, mchezaji huyo alisisitiza kuwa hayo yalikuwa ni maamuzi yake binafsi.
Burke aliongeza kuwa, waliamua kuwahamisha wachezaji waliamua kubakia nchini Australia, baada ya ubalozi wa Iran kugundua mahali ilipo hoteli walipofikia.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Iran, lilidai kuwa Australia iliwashinikiza wachezaji hao kuomba hifadhi ya kisiasa nchini humo.
Viza kwa wachezaji hao, zilitolewa siku ya Jumanne, siku moja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuisihi Australia kuwapa wachezaji wa Iran hifadhi ya kisiasa, akisema kuwa wachezaji hao watakuwa hatarini pindi watakaporudi nchini mwao.
Iran ilikuwa inashiriki michuano ya Kombe la Bara la Asia kwa upande wa wanawake, lililokuwa likifanyika nchini Australia, kabla ya kutolewa.













