Raia wa Uganda wanaelekea katika vituo vya kupigia kura siku ya Alhamisi Januari 15, 2026 chini ya ulinzi mkali katika mji mkuu wa Kampala, huku wanajeshi na polisi wakiwa kwenye maeneo ya miji na wengine wakishika doria katika vituo vya kupigia kura.
Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, zoezi la kuanza kupiga kura linaripotiwa kuchelewa.
Rais Yoweri Museveni, 81, anataka kuongeza muda wa utawala wake wa takriban miongo minne katika kinyang'anyiro dhidi ya kiongozi wa chama cha upinzani Bobi Wine. Mamlaka nchini humo imesitisha kwa muda huduma ya mtandao wa simu. Tume ya Mawasiliano imedai hatua hiyo itasaidia kuzuia kusambaa kwa taarifa potofu ambazo zinaweza kuleta taharuki kwa wananchi.
Vikosi vya usalama vimeripotiwa kuwafyatulia risasi mara kwa mara watu wakati mgombea wa upinzani Bobi Wine akifanya kampeni, na kuua mtu mmoja, na kuwakamata mamia ya wafuasi wake.
Serikali ya Museveni imetetea hatua ya vikosi vya usalama dhidi ya wananchi na kusema imesababishwa na uvunjaji wa sheria.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema wiki iliyopita kuwa uchaguzi huo ulikuwa unafanyika huku kukiwa na "ukandamizaji na vitisho."
Kando na Wine, wagombea wengine sita wa upinzani wanawania nafasi ya urais.
Wapiga kura pia watachagua zaidi ya wabunge 500 pia.
Zoezi la upigaji kura linatarajiwa kukamilika saa kumi jioni huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa ndani ya saa 48, yaani kufikia Jumamosi alasiri.














