Ni kama fainali yenyewe, ila ni nusu fainali ikiwa marudio ya fainali ya AFCON 2021. Mafarao wanahitaji mafanikio baada ya ukame wa miaka 16 AFCON.
Baada ya kushinda mara tatu mfululizo 2010, Misri imemaliza katika nafasi ya pili mara mbili, 2017 walipofungwa na Cameroon na 2021 kwa Simba wa Teranga.
Kwa kile kinachoonekana kama pengine yakawa mashindano ya mwisho ya mshambuliaji Mohamed Salah, Misri inatarajia kuwa yatakuwa mazuri kumuaga na ushindi.
Salah ameshinda mataji mengi makubwa, ikiwemo Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hajawahi kutia kunyanyua kombe la AFCON na ana hamu sana kufanikisha hilo kabla kutundika daluga.
Mechi zilizochezwa kati ya wababe hao wawili wa Afrika tangu 2014 mara nyingi Simba wa Teranga wameibuka kidedea. Misri imeshinda moja kati ya tano ambapo ni ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022.
Misri itakuwa inacheza nusu fainali yake ya tatu katika makala tano zilizopita. Kwa Senegal, itakuwa ya tatu kati ya makala nne.
Nusu fainali nyingine itakuwa kati ya Nigeria na Morocco.















