Israel imeiarifu Umoja wa Mataifa kwamba itaruhusu malori 300 tu ya misaada kuingia Gaza kuanzia Jumatano, nusu ya idadi iliyokubaliwa, na kwamba hakuna mafuta au gesi yatakayoruhusiwa kuingia katika eneo hilo isipokuwa kwa mahitaji maalum yanayohusiana na miundombinu ya kibinadamu, kulingana na taarifa iliyoonwa na Reuters na kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa.
Olga Cherevko, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu huko Gaza, alithibitisha Jumanne kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa umepokea taarifa hiyo kutoka COGAT, kitengo cha jeshi la Israel kinachosimamia "mtiririko wa misaada" kuelekea Gaza.
COGAT ilisema Ijumaa kwamba ilitarajia takriban malori 600 ya misaada kuingia Gaza kila siku wakati wa kusitisha mapigano.
Hapo awali, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu walitoa wito wa kufunguliwa kwa mipaka yote kuelekea Gaza ili kuruhusu misaada inayohitajika sana kuingia katika eneo la Palestina.
Walisema kwamba usitishaji mapigano dhaifu huko Gaza, ulioanzishwa chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump, unahitaji kuona mipaka ikifunguliwa ili kupeleka misaada kwa wingi katika eneo hilo lililoathiriwa na njaa.
Msemaji wa shirika la kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA, Jens Laerke, aliongeza, "Tunahitaji mipaka yote kufunguliwa."
Laerke alisema kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa na tani 190,000 za misaada tayari kusafirishwa kuingia Gaza.