Burkina Faso: Kiongozi wa kijeshi Ibrahim Traore ajiongezea miaka mitano ya utawala

Burkina Faso: Kiongozi wa kijeshi Ibrahim Traore ajiongezea miaka mitano ya utawala

Kiongozi huyo wa kijeshi atabakia madarakani mpaka 2029, na hivyo kuchelewesha mchakato wa nchi hiyo kuongozwa kidemokrasia.
Ibrahim Traore aliingia madarakani Septemba 30, mwaka jana. /Picha: AA

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso itasalia madarakani kwa miaka mingine mitano kufuatia majadiliano ya Jumamosi.

Uongozi huo ulitwaa madaraka kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2022 na kuahidi kuendesha uchaguzi wa kidemokrasia mwezi Julai mwaka huu ambao ungeanzisha utawala wa kiraia.

Kulingana na makubaliano hayo yaliyotiwa saini na kiongozi wa kijeshi Ibrahim Traore, mabadiliko hayo yatasubiri miezi 60 kutoka Julai 2.

"Uchaguzi unaoashiria mwisho wa kipindi cha mpito unaweza kupangwa kabla ya tarehe hii ya mwisho ikiwa hali ya usalama inaruhusu," ilisomeka sehemu ya makubaliano hayo.

Mfululizo wa mapinduzi

Ucheleweshaji huo mkubwa huenda ukaongeza wasiwasi kuhusu kurudi nyuma kwa demokrasia katika ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, ambako umeshuhudia mapinduzi manane katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Katiba hiyo pia inamruhusu Traore kugombea urais wakati wa uchaguzi huo.

Ghasia katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi zilizochochewa na mapigano ya muongo mmoja na makundi ya kigaidi yenye mafungamano na al Qaeda na Daesh zimezidi kuwa mbaya tangu wanajeshi kunyakua madaraka nchini Burkina Faso na nchi jirani za Mali na Niger.

Burkina Faso imeshuhudia ongezeko kubwa la mauaji kwa mwaka 2023, huku watu zaidi ya 8,000 wakiripotiwa kufa, kulingana na taasisi ya Kimarekani ya ACLED.

TRT Afrika