| Swahili
AFRIKA
2 DK KUSOMA
Jeshi la Polisi Tanzania laimarisha ulinzi siku chache kabla ya maandamano
Hatua hiyo inafuatia tamko lililotolewa na Chama cha CHADEMA la kuandamana siku ya Septemba 23, 2024.
Jeshi la Polisi Tanzania laimarisha ulinzi siku chache kabla ya maandamano
Kikosi cha Kutuliza Ghasia nchini Tanzania./Picha: Reuters / Others
21 Septemba 2024

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeimarisha ulinzi katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, siku chache kabla maandamano ya chama cha upinzani cha CHADEMA.

Ulinzi huo umeimarishwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, huku CHADEMA wakiwa wameazimia kufanya maandamano yao ya Septemba 23, 2024.

Magari ya Kikosi cha Kutulia Ghasia cha Jeshi la Polisi Tanzania, maarufu kama FFU yalionekana yakizunguka maeneo tofauti ya jiji hilo la kibiashara nchini Tanzania.

Wakati huo huo, chama cha CHADEMA kimesisitiza nia yake ya kuendelea na maandamano hayo yenye lengo la kupinga, kulaani na kuitaka serikali ya Tanzania ikomeshe mara moja wimbi la watu kutewa, kupotezwa, kuumizwa na wengine kuuwawa kiholela.

Chama hicho, pia kimeitaka serikali ya nchi hiyo kupitia Jeshi la Polisi Tanzania kuwarejesha viongozi wake ambao kinadai wametekwa na hawajulikani walipo, licha ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa amri kwa Jeshi hilo kuwatafuta.

“Tunawakaribisha wananchi wote wajitokeze kwa wingi tuandamane kwa amani na kufikisha maombolezo na kilio chetu ili kwa pamoja tuweze kukomesha mauaji haya ya kiholela nchini, hakuna ambaye yuko salama miongoni mwetu,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Afisa habari wa CHADEMA kwa kanda ya pwani, kama ilivyochapishwa kwenye ukurasa wa X wa chama hicho.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika