Programu hiyo imetwaa tuzo ya kimataifa./Picha: Wengine

Na Kevin Philips Momanyi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Programu maalumu yenye kutoa tiba ya kisaikolojia ya Thalia Psychotherapy kutoka Kenya imeshinda tuzo ya afya wakati wa mkutano wa kimataifa wa teknolojia wa Viva 2024 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa hivi karibuni.

Mkutano huo mkubwa ulimwenguni, ulikuwa pia ni kama jukwaa la kujadiliana namna bunifu mbalimbali, hasa za Akili Mnemba zinavyoweza kuleta suluhisho kwa maisha ya binadamu.

Akizungumza kwenye tukio hilo, mwanzilishi mwenza na mkuu wa mikakati kutoka Thalia Psychotherapy Antony Okungu, aliweka wazi nia ya kuongeza wigo wa programu hiyo, hususani baada ya kutambuliwa kimataifa.

“Kutambuliwa huku kunaongeza dhamira yetu ya kueneza huduma zetu za kinga za afya ya akili kote Afrika,” alisema.

Pia alisisitiza lengo la kuongeza upatikanaji wa suluhu za afya ya akili katika bara zima la Afrika.

Mkutano huo mkubwa ulimwenguni, ulikuwa pia ni kama jukwaa la kujadiliana namna bunifu mbalimbali, hasa za Akili Mnemba zinavyoweza kuleta suluhisho kwa maisha ya binadamu./Picha: Wengine

Kwa upande wake, Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Thalia Psychotherapy, Mercy Mwende amesema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya kukubalika kwa teknolojia hiyo katika kutatua changamoto ya afya ya akili barani Afrika.

“Ni imani yetu kuwa hata hospitali na taasisi zingine za afya zitakuwa tayari kufanya kazi na sisi,” ameeleza.

Programu hiyo yenye kutoa tiba ya kisaikolojia imeshinda tuzo ya kimataifa katika kipengele cha afya huko nchini Ufaransa hivi karibuni./Picha: Wengine

Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya maendeleo Chrysoula Zacharopoulou, alipongeza programu hiyo akisema kuwa inaonesha namna ambavyo bara la Afrika linaweza kupata suluhu kubwa, kushughulikia changamoto kubwa ya afya ya akili na nishati na mawazo mapya.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), mzigo wa afya ya akili husababisha matatizo kadhaa kama vile msongo wa mawazo, kujiua na matumizi mabaya ya pombe na mihadarati , na kufanya matatizo ya akili kuwa moja ya changamoto kubwa kwa nchi nyingi duniani na huchangia kuwaweka vijana kwenye hatari kama ya kufanya ngono isiyo salama, na hata uendeshaji mbaya wa vyombo vya moto.

TRT Afrika