Mwanajeshi wa Sudan People's Liberation Army (SPLA) akiwa katika ulinzi katika kambi ya Umoja wa Mataifa huko Abyei./ Picha : Reuters 

Mashambulizi ya makundi hasimu ya kabila la Dinka katika eneo linalodaiwa na Sudan na Sudan Kusini yaliwauwa takriban watu 32 mwishoni mwa juma, afisa mmoja wa eneo hilo alisema Jumatatu.

Vurugu vimekuwa vikizuka mara kwa mara katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei, ambapo kabila la Twic Dinka kutoka Jimbo jirani la Warrap nchini Sudan Kusini wamefungwa kwenye mzozo na Ngok Dinka kutoka Abyei kuhusu eneo la mpaka wa kiutawala.

Duru zinaarifu kuwa Jumapili asubuhi, vijana wa Twic Dinka waliokuwa na silaha, wakiungwa mkono na wanamgambo wa eneo hilo, walishambulia vijiji kadhaa vya Ngok Dinka kaskazini mashariki mwa mji wa Agok, Bulis Koch, waziri wa habari wa eneo la Tawala la Abyei, aliiambia Reuters.

''Wanaume waliovalia sare za jeshi la Sudan Kusini, wakiungwa mkono na wapiganaji wa Twic Dinka, pia walishambulia makazi ya Ngok Dinka,'' Koch alisema.

Shirika la Reuters linasema kuwa juhudi zao za kupata majibu kutoka kwa Wasemaji wa jeshi la Sudan Kusini hazikufua dafu.

Katika taarifa yake Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa cha Abyei (UNISFA) kimelaani mashambulizi hayo na kusema kimeimarisha usalama katika eneo hilo kwa kuimarisha doria na kushirikisha uongozi wa kisiasa wa Abyei na viongozi wa kimila ili kutuliza mivutano.

Kamanda wa kikosi cha UNISFA alizitaka "jamii zote kujiepusha na ghasia na kujitolea kuhakikisha amani endelevu Abyei," ilisema taarifa hiyo.

Abyei imekuwa ikivutaniwa na Sudan na Sudan Kusini tangu nchi hiyo ilipojitangazia uhuru wake mwaka 2011. Abyei ilikuwa na hadhi maalum ya kiutawala, ikitawaliwa na utawala unaojumuisha maafisa walioteuliwa na Juba na Khartoum.

TRT Afrika na mashirika ya habari