Marekani imelaani vikali shambulizi la Ijumaa ambalo liliua takriban watu tisa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa yake/ Picha : Reuters 

Rwanda siku ya Jumamosi ilikanusha shutuma za Marekani kwamba vikosi vyake vilishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na badala yake kuwalaumu wanamgambo iliyosema wanaungwa mkono na jeshi la Congo kwa shambulio hilo.

Marekani imelaani vikali shambulizi la Ijumaa ambalo liliua takriban watu tisa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa yake.

''Mashambulizi hayo yalifanywa kutoka maeneo ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda,'' taarifa ya Marekani ilisema. ''Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu upanuzi wa hivi karibuni wa RDF na M23 Mashariki mwa Congo,'' iliendelea kusema.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alikanusha kuwa RDF ilihusika na shambulio hilo na badala yake alilaumu wanamgambo wanaoungwa mkono na jeshi la Congo.

"RdF, jeshi la kitaaluma, halitawahi kushambulia IDP (kambi za wakimbizi),'' alisema Makolo. ''Wachunguzeni hao waasi wa FDLR na Wazalendo wanaoungwa mkono na FARDC (jeshi la Kongo) kwa ukatili wa aina hii," Makolo aliandika kwenye chapisho X.

Katika chapisho hilo, Makolo alikuwa akimjibu Mathew Miller, msemaji wa serikali ya Marekani kufuatia tuhuma zake.

Kundi la FDLR ni kundi la Wapiganaji lililoanzishwa na maafisa wa Kihutu waliokimbia Rwanda baada ya kufanya mauaji ya halaiki ya 1994 huku kundi linalojiita Wazalendo wakiwa wanamgamboi wa dhehebu la Kikristo.

Mashambulizi ya miaka miwili ya waasi wa M23 yamesonga karibu na mji wa Goma mashariki mwa Kongo katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha maelfu ya watu kutafuta hifadhi katika mji huo kutoka maeneo jirani.

TRT Afrika na mashirika ya habari