Waandaaji wa tuzo za dunia za Guinness wamekana kumtambua mpishi huyo./Picha:Smith/Facebook

Na Charles Mgbolu

Ndoto za mpishi Ebenezer kutoka Ghana za kuingia kwenye vitabu vya rekodi za dunia zimeyeyuka.

Siku ya Jumanne, vyombo vya habari nchini Ghana viliripoti kuwa Smith alivunja rekodi ya dunia ya upishi.

“Leo ni siku kubwa ambayo itabakia katika kumbukumbu zangu. Najisikia kuwa mwenye heshima sana, kuwa kama sehemu ya orodha ya rekodi za dunia," alisema Smith katika mkutano na vyombo vya habari mjini Accra.

Kwa namna ya pekee, Smith alipata wasaa wa kuonesha cheti alichopata kutoka kwa waandaaji wa tuzo za dunia za Guinness, wakitambua mafanikio yake.

Mpishi huyo anadai kuwa alitambuliwa na waandajaji wa tuzo dunia za Guinness. Picha:  Smith/Facebook

Lakini katika hali ya kushangaza, waandaaji wa tuzo hizo wamekanusha kuwahi kumuidhinisha Smith kama mpishi anayeshikilia rekodi.

Kulingana na waandaaji wa tuzo za Guinness, zawadi hiyo ilikuwa ni ya bandia.

“Hapana, hii si kweli kabisa. Hatujatoa tuzo kama hiyo wala si yeye anayeshikilia rekodi hiyo. Kwa sasa, anayeshikilia rekodi hiyo ni Alan Fisher kutoka Ireland," walisema waandaaji wa tuzo za Guinness katika taarifa yao.

Smith anadai kuwa alikabidhiwa tuzo hiyo kwa kuweza kupika chakula kwa muda wa saa 820 na dakika 25, kutoka Februari 1 mpaka Machi 6, 2024.

Mpishi huyo hakuwa tayari kuzungumzia sakata hilo./Picha: 

Katika mtandao wake, waandaji wa tuzo hizo wanasema kuwa rekodi ya "marathoni ndefu zaidi ya kupikia (ya mtu binafsi) ni saa 119 na dakika 57 sekunde 16 na ilifikiwa na Alan Fisher huko Matsue, Shimane, Japani, kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 3 Oktoba 2023.

Walienda mbali na kuondoa kipengele hicho kwenye tovuti yake, na ujumbe sasa ukisomeka, "Rekodi hii haitumiki kwa sasa na hakuna maombi yanayokubaliwa kwa ajili yake."

Ebenezer Smith amejaribu kufanya hivyo baada ya mpishi mwingine wa Ghana, Failatu Abdul Razak, kujaribu na kushindwa.

Katika mahojiano na kituo cha redio cha Accra, meneja wa mpishi huyo, Benny amesema kuwa hakuwa anafahamu uwepo wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo na kwamba alikuwa na barua pepe kutoka kwa waandaaji hao ikimthibitisha Smith, kama mshikiliaji mpya wa rekodi hiyo ya dunia.

TRT Afrika