Wapiga kura milioni 28 wa Afrika Kusini waliojiandikisha wana nafasi ya kuchagua wawakilishi katika mabunge ya kitaifa na majimbo. Picha / Reuters

Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa waangalizi wa uchaguzi wamewasili Afrika Kusini kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 29 Mei 2024.

Wapiga kura milioni 28 wa Afrika Kusini waliojiandikisha watakuwa na nafasi ya kuchagua wawakilishi katika mabunge ya kitaifa na majimbo.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, aliidhinisha kutumwa kwa waangalizi hao kwa muda mfupi ili kutathmini na kutoa ripoti kuhusu mwenendo wa uchaguzi huu.

"Timu ya AU inaongozwa na Uhuru Kenyatta, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kenya na inajumuisha waangalizi 60 wa muda mfupi kutoka mabalozi walioidhinishwa na Umoja wa Afrika, maafisa wa mashirika ya usimamizi wa uchaguzi.

Pia ina wanachama wa mashirika ya kiraia ya Afrika, wataalamu wa uchaguzi wa Afrika, haki za binadamu. wataalamu wa masuala ya jinsia na vyombo vya habari, na wawakilishi wa mashirika ya vijana," " taarifa ya Umoja wa Afrika imesema.

Waangalizi hao wametolewa kutoka nchi 24 ambazo ni pamoja na Angola, Benin, Botswana, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, Eswatini, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mauritius, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Sudan Kusini, Togo, Tunisia, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Timu ya waangalizi wa Uchaguzi Afrika Kusini inaongozwa na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta / Picha: Ofisi ya rais wa 4 wa Kenya. 

Jukumu la waangalizi

Kulingana na Umoja wa Afrika, AU, jukumu la waangalizi wake uchaguzi katika Umoja wa Afrika ni pamoja na:

  • Kutoa ripoti au tathmini sahihi na isiyo na upendeleo ya uchaguzi, ikijumuisha kiwango ambacho uendeshaji wa uchaguzi unakidhi viwango vya kikanda, bara na kimataifa vya uchaguzi wa kidemokrasia
  • Kutoa mapendekezo ya kuboresha uchaguzi ujao kwa kuzingatia matokeo
  • Kuonyesha nia ya AU ya kuunga mkono uchaguzi wa nchi wanachama wa AU
  • Ni mchakato wa demokrasia, ili kuhakikisha kwamba uendeshaji wa uchaguzi wa kweli unachangia uimarishaji wa utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu.

Wajumbe hao watafanya majadiliano na mamlaka za serikali, Tume Huru ya Uchaguzi, vyama vya siasa, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa. Ujumbe huo pia unatarajiwa kukutana na timu nyengine za waangalizi wa uchaguzi zilizotumwa kuchunguza Uchaguzi Mkuu wa 2024 nchini Afrika.

Timu hiyo itatoa taarifa kuhusu maoni yake kwa uchaguzi huo na mapendekezo yake kuhusu uendeshaji wa uchaguzi tarehe 31 Mei 2024 katika mkutano na waandishi wa habari huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Watatarajiwa kutoa ripoti yao ya mwisho na ya kina ndani ya miezi miwili kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi. Ripoti hii itawekwa kwenye tovuti ya Tume ya AU.

Uchaguzi wa saba

Huu utakuwa uchaguzi ya saba tangu kuanza kwa enzi ya demokrasia mwaka 1994.

Wananchi huwa hawampigi kura rais.

Badala yake wanachagua wajumbe 400 wa bunge la Kitaifa, ambao wanakwenda kumpigia kura kiongozi mpya wa nchi ndani ya siku 30 za uchaguzi mkuu.

Chama cha Africa National Congress , ANC, ambacho kimeongoza tangu 1994 kinatetea nafasi yake tena katika uchaguzi huu.

TRT Afrika