Yanga wameweka rekodi nzuri katika mechi zao za nje kwa hiyo wanatazamiwa kuwa na fursa nuri ya kujikomboa : Picha Yanga FC

Timu ya Tanzania Yanga FC wanaingia uwanjani Jumamosi wakitafuta kukomboa sura katika mechi ya mwisho ya fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya wenyeji USM Alger wa Algeria.

Yanga wanatafuta kulipiza kisasi kutokana na pigo la 2-1 waliopewa nyumbani Dar Es Salaam, Tanzania, walipokutana katika duru ya kwanza ya fainali hiyo, ilimradi wafike hata kama ni mikwaju ya penalti, ila lazima angalau wasawazishe mizani.

Lakini mchambuzi wa soka Tanzania Ramadhan Mbwaduke anasema kuwa watakuwa na kibarua kigumu.

‘‘Katika utaratibu wa fainali kama hii ya mechi mbili, anayeshinda ugenini anakuwa na nafasi bora zaidi kunyakua kombe, na USM wanao ushindi wa ugenini.’’ Amesema Ramadhan. ‘’Lakini hilo silo tisho kwa Yanga kwani wanayo fursa nzuri ya kujikwamua. Ila kibarua kigumu maana ya mazingira ya ugenini sio kama ya nyumbani.’’

Yanga watalenga kujirekebisha mapungufu yao ya Dar, wanapo onana na wapinzani wao USM Alger.

‘‘Kilicho wakwaza jijini Dar, unakuta Mayele anacheza mbele kushoto na anakuja kugongana huko na Musonda,’’ anasema Ramadhan. ‘‘Sasa inakuwa hakuna mtu wa kumpokea kumalizia mikwaju wavuni. Na ndilo tatizo pia lilitokea kulia.’’

Ramadhan anasema lazima Yanga wajitahidi kuondoa hatari langoni.

‘‘Unapocheza mechi kama hii unatakiwa hizi foul usilete karibu na lango lenu.’’ Anasema Ramadhan. ‘’Foul ni lazima zitakuwepo hasa wanapoona hatari, ila wafanye bidi wacheze juu wasilete hatari langoni kwao.’’

Yanga wameonesha rekodi nzuri zaidi katika mechi zao za nje, huku takwimu zikionesha kuwa kati ya mechi 5 walizocheza ugenini, tatu walishinda na kutoka sare moja. Hii inawapa nguvu ya mechi za ugenini kwa 97%.

Lakini USM Alger watakuwa na bahati ya kucheza nyumbani kwa hiyo watakuwa na hamasa zaidi ya kujionesha mbele ya mashabiki wao. Pia kumbuka hawajafungwa hata mechi moja waliocheza nyumbani.

‘‘Mayele ni mshambuliaji hodari sana. Lakini Algeria wanajua hilo na ninatarajia watamkaba muda wote,’’ anasema Ramadhan, ‘‘Hapo ndipo wanatakiwa Yanga kutumia fursa hiyo kuwapenyeza washambuliaji wengine kama Musonda, Aziz au Salum.’’

Mayele ametajwa kuwa chombo muhimu cha Yanga mchuano huu, kwani kati ya mabao 17 ambazo Yanga wametinga, saba ni za Mayele huku akisaidia kwa mabao 3.

Kwa mujibu wa Ramadhan, Yanga wanayo fursa 50 kwa 50, ya kushinda kombe hilo, ‘’Muhimu ni wawe makini, na wajaribu kuwakimbiza Algeria mbio ambayo hawajaona.’’ Anashauri Ramadhan.

TRT Afrika