Ruth Chepngetich, mshindi maarufu wa mbio za Chicago Marathon 2024 na mmiliki wa rekodi ya dunia kutoka Kenya, amepigwa marufuku ya miaka mitatu baada ya kubainika kutumia dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku, hydrochlorothiazide (HCTZ).
Sampuli yake ya mkojo iliyochukuliwa mwezi Machi ilionyesha kiwango cha dawa hiyo kilichozidi kiwango kinachoruhusiwa mara 190.
Kitengo cha Uadilifu wa Riadha (AIU) kimethibitisha adhabu hiyo huku ikisisitiza kwamba mafanikio na rekodi zake zote kabla ya Machi 14, 2025 zitaendelea kutambuliwa.
Awali, mwanariadha huyo alikana kabisa kutumia dawa hiyo, akisema “hakuwa na maelezo yoyote kuhusu matokeo ya kipimo hicho”, na akasisitiza kwamba hajawahi kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Hata hivyo, baadaye alibadilisha kauli yake, akidai kwamba alikuwa amekunywa dawa za mfanyakazi wake wa nyumbani baada ya kuugua siku mbili kabla ya kipimo hicho — jambo ambalo alisema alishindwa kulieleza kwa wachunguzi wa AIU.
AIU ilisema maelezo hayo mapya “hayaaminiki kabisa.”
Orodha ndefu ya waliopigwa marufuku
Adhabu ya Chepngetich inaongeza idadi ya wanariadha wa Kenya waliopigwa marufuku, ikiwemo majina makubwa kama Jemima Sumgong, mshindi wa dhahabu wa marathon katika Olimpiki ya 2016.
Tangu mwaka 2017, zaidi ya wanariadha 140 wa Kenya wamepigwa marufuku na AIU — idadi kubwa zaidi kuliko taifa lolote.
Baada ya kashfa nyingi, Kenya imewekeza mamilioni ya pesa kukabiliana na tatizo la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu.
Shirika la Dunia la Kupambana na Dawa za Kulevya Michezoni (WADA) limesema mapema mwezi huu kuwa Kenya imeonyesha “mafanikio makubwa” katika kusafisha mfumo wake.












