Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatano, Serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump ilidai kuwa maafisa wa Somalia waliiba tani 76 za chakula cha misaada kilichotolewa na wafadhili, ambacho kilikuwa kimekusudiwa kuwasaidia Wasomali wenye uhitaji.
Katika chapisho hilo Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani waliwakemea viongozi wa Somalia Siku ya Jumatano na kutangaza kusitisha "mipango yote inayoendelea ya usaidizi ya Marekani" kwa serikali ya Somalia.
Maafisa wa Marekani waliongeza kuwa msaada wowote katika siku zijazo "utategemea Serikali ya Somalia kuwajibika" na kurekebisha suala hilo.
Hadi sasa, maafisa wa Somalia hawajajibu madai hayo ya wizi wa misaada.
Operesheni dhidi ya wahamiaji Minnesota
Katika wiki za hivi karibuni serikali ya Trump imewasuta mara kwa mara Wasomali nchini Marekani, ikiwalenga katika uvamizi wa wahamiaji huko Minnesota na kudai ulaghai mkubwa wa manufaa ya umma katika jumuiya ya Wasomali katika jimbo hilo la katikati ya magharibi, ambalo ni kubwa zaidi nchini humo lenye takriban Wasomali 80,000.
Mnamo Novemba, Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa hadhi ya ulinzi wa muda kwa wahamiaji wa Somalia, akiwashutumu kwa vurugu za magenge, akiongeza "warudishwe walikotoka."
Hatua hiyo pia inakuja baada ya kuzuka kwa mzozo kati ya Somalia, Marekani na washirika wa Washington nchini Israel.
Israel ilitangaza mwezi uliopita kulitambua rasmi eneo lililojitenga la Somaliland, utambuzi wa kwanza kwa eneo hilo tangu lilipojitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991.
Nafasi ya Somaliland kwenye Ghuba ya Aden, ukaribu na maadui wa Israel nchini Yemen, unaifanya eneo hilo kuwa na umuhimu wa kimkakati.















