Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir ana imani kuwa taifa hilo litafanya uchaguzi wake baadaye mwaka huu, baada ya mchakato huo kucheleweshwa mara kwa mara.
Miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, taifa la Sudan linaigia katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Disemba 22, 2026.
Katika tangazo lake la Septemba 22, Rais Salva Kiir alisema kuwa, matayarisho yote yamefanyika kwa ajili ya mchakato huo muhimu katika historia la taifa hilo changa duniani.
Licha ya kuhairishwa mara kwa mara, Rais Salva Kiir anaamini kuwa, nchi yake ipo tayari kwa mchakato huo kwa mustakabali wa demokrasia ya nchi hiyo.
Kuondolewa kwa Manaibu Rais
Septemba 22 mwaka huu, kiongozi huyo alitangaza kuwafuta kazi, manaibu zake watano, ambao ni Riek Machar, James Wani Igga, Taban Deng Gai, Rebecca Nyandeng De Mabior, na Hussein Abdelbagi Akol, kama hatua ya kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Uamuzi huo, ulikuwa ni sharti muhimu kuelekea mchakato wa uchaguzi, kulingana na sheria mpya ambayo ilipingwa na chama cha Machar, kwa madai kuwa inakiuka mkataba wa amani wa mwaka 2018.
Kwa sasa, Machar yupo kwenye kizuizi cha nyumbani, akikabiliwa na tuhuma za uhaini.
Hatua, imeibua sintofahamu Sudan Kusini, huku vurugu zikishuhudiwa katika eneo la Jonglei ya Kati.
Ulinzi kuimarishwa
Hali hiyo ya sintofahamu, imelazimu serikali ya nchi hiyo kuweka ulinzi mkali katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Hata hivyo, licha ya imani iliyooneshwa na serikali, bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili Sudan Kusini itemize ndoto ya kuwa na uchaguzi wa huru na wa haki.
Kwa mfano, mchakato huo wa uchaguzi unatarajiwa kuigharimu nchi hiyo kiasi cha Dola milioni 250, huku tume ya uchaguzi ya Sudan Kusini ikiwa imepokea Dola milioni 27 pekee.
"Tunaweza kukosa uchaguzi tena mwaka huu, hasa ukizingatia kuwa kuna mambo mengi ambayo bado hayajakamilishwa hadi kufikia sasa,” anatahadharisha Gordon Odhiambo, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa kutoka Kenya, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Maoni yake yanaungwa mkono Abraham Nyuon, profesa wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Sudan Kusini.
"Hivi karibuni, taifa hilo limefanya mabadiliko katika tume ya uchaguzi, jambo linaloashiria kuwa Gabriel Bol Deng atahitaji muda zaidi ili aweze kuzeoa majukumu yake mapya,” anaeleza.
Mwanazuoni huyo, anabainisha kuwa, vurugu za kisiasa zinaweza kuzorotesha kufanyika kwa uchaguzi wa haki na huru nchini humo.
Mwanzo mpya
Hata hivyo, kulingana na Profesa Nyuon, mchakato wa uchaguzi ujao wa Sudan Kusini, ni fursa pekee kwa taifa hilo changa, kupiga hatua na kusonga mbele.
"Kwa muda mrefu sasa, maslahi binafsi yamedhoofisha maendeleo ya Sudan Kusini. Ni imani yangu kuwa, licha ya kuwa na kesi mahakamani, bado kuna fursa ya kujijenga upya."
Licha ya changamoto za kisiasa nchini humo, Odhiambo anasisitiza umuhimu wa wanasiasa waandamizi nchini humo, akiwemo Rais Kiir mwenyewe na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maachar kukaa chini pamoja, ili kuwepo mabadiliko salama ya kisiasa na kiuongozi.
"Watakapozungumza kauli moja, basi viongozi hao wanaweza wakaleta ushawishi mkubwa siku ya uchaguzi,” alisema Odhiambo.
Hata hivyo, upinzani unamtuhumu Kiir kwa vitendo vyake visivyo vya kiungwana, hususani mara baada ya kuwafukuza kazi manaibu zake, bila kuzingatia mkataba wa amani wa 2018.
Chama cha SPLM-IO, kinadai kuwa kitendo cha Kiir kinalenga kuzidi kumpa madaraka yeye mwenyewe.
"Ujenzi mpya wa taifa, unahitaji mazungumzo na wapinzani wako wa kisiasa,” kilisema chama hicho kupitia taarifa yake ya Septemba 23.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu
Mara baada ya uhuru wake, Sudan Kusini ilishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vilisababisha vifo vya watu wapatao 400,000.
Hali kadhalika, taifa hilo lilipanga kuwa na uchaguzi wake Disemba 2024, lakini ikashindikana kutokana na ukosefu wa fedha, pamoja na kuahirishwa kwa chaguzi za 2018, 2021, na 2023.





















