Utajiri wa Afrika: Vyungu maalum vya Botswana
Utengenezaji wa vyungu tangu jadi ni ufundi wa wanawake hasa ndani ya jumuiya inayoitwa Bakgatla ba Kgafela nchini Botswana/ picha: UNESCO / Public domain
Utajiri wa Afrika: Vyungu maalum vya Botswana
Kinachofanya ufinyanzi wa Botswana kuwa wa kipekee ni kuanzia kile wanachoamini kuwa ni muongozo kutoka kwa mababu katika ukusanyaji wa udongo.
tokea masaa 2

Katika jamii zetu za kiafrika matumizi ya vyungu vya udongo ni ya kawaida tu, lakini ukienda nchini Botswana vyungu vya udongo ndivyo vinavyothaminiwa sana.

Tangu jadi ni ufundi unaotawaliwa na wanawake, hasa ndani ya jumuiya inayoitwa Bakgatla ba Kgafela ambayo inajishughulisha na ufundi huu wa vyungu vinavyotengezwa kwa mikono.

Vyungu hutumika kuhifadhi maji na kupika.

Wanawake hutumia udongo, samadi ya ng'ombe, na oksidi ya chuma.

Vyungu vyenye maumbo, miundo na mitindo tofauti vinavyotengenezwa vinavyohusiana na mila na imani za jamii.

Kinachofanya ufinyanzi wa Botswana kuwa wa kipekee ni kuanzia kile wanachoamini kuwa ni muongozo kutoka kwa mababu katika ukusanyaji wa udongo.

Wakati wa kukusanya udongo, mfinyanzi mkuu huwasiliana na mababu kupitia muda wa kutafakari ili aweze kuongozwa hadi mahali panapofaa.

Baadaye mchanga na udongo huchanganywa kwa kutumia kinu na mti wake, kisha huchujwa na kuchanganywa na maji ili kuunda umbo la chungu.

Vyungu kutengenezwa kwa mikono katika maumbo ya duara au mviringo.

Baada ya kupambwa, chungu huchomwa kwenye tanuri ili kukauka.

Ujuzi wa vyombo vya udongo hupitishwa kwa watoto wa kike na wajukuu wa kike.

Hata hivyo, sasa utamaduni huu wa kipekee kwa watu wa Botswana uko katika hatari ya kutoweka kwa sababu ya kupungua kwa idadi ya wafinyanzi wakuu.

Pia bidhaa zilizomalizika hazivutii tena bei  kubwa huku changamoto kubwa ikiwa ni ya watu kutaka vyombo vya kisasa vilivyotengenezwa kwa chuma, glasi au plastiki.

Mwaka wa 2012 ujuzi huu wa ufinyanzi wa udongo- katika wilaya ya Kgatleng ya Botswana ulitambuliwa na Shirika la UNESCO kama urithi ambao unahitaji kulindwa.

CHANZO:TRT Swahili