Hatua kubwa ya mpango wa Uturuki wa kuwa na “Uturuki isiyokuwa na ugaidi” imepigwa siku ya Jumapili wakati kundi la kigaidi la PKK lilipotangaza kuwa linaondoa wapiganaji wake kutoka nchini Uturuki hadi kaskazini mwa Iraq.
Kundi la kigaidi la PKK limesema katika taarifa iliyosomwa eneo la Qandil la Sulaymaniyah, kaskazini mwa Iraq kuwa linatekeleza mpango wa kuondoa vikosi vyake vyote kutoka Uturuki.
Taarifa hiyo inasema uamuzi wa kuondoa kabisa kundi hilo la kigaidi lenye silaha na shughuli zake ulichukuliwa mwezi Mei kupitia maagizo ya kiongozi wao aliyefungwa jela, Abdullah Ocalan.
Kundi la magaidi 23 wa PKK ambao wanasemekana walisafiri kutoka Uturuki walikuwepo wakati wa tangazo hilo kwenye sehemu hiyo.
Mwezi Julai, kundi la wanachama wa PKK liliharibu sehemu ya kwanza ya silaha zao, hatua ambayo Uturuki iliieleza kuwa "muhimu ambayo haiwezi kubadilika".
Kundi hilo, ambalo limetajwa kuwa la kigaidi na Uturuki, Marekani na EU, limekuwa likishambulia Uturuki katika vita vya kigaidi kwa miongo kadhaa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu tangu kwenye miaka ya themanini.
Efkan Ala, Makamu Mwenyekiti wa Chama tawala cha Haki na Maendeleo (AK), anasema matangazo ya sasa na hatua zilizochukuliwa ni “hatua muhimu zilizokuwa zimebaki katika kuangamiza ugaidi.”
“Kwa kuangamiza kabisa ugaidi, ambao umekuwa changamoto kubwa kwa taifa letu, milango ya enzi mpya imefunguliwa," alisema.
Msemaji wa chama cha AK Omer Celik anasema shughuli inayoendelea ya kuwapokonya silaha na kuvunja mifumo ya silaha ya PKK nchini Uturuki, Iraq na Syria ni matokeo ya mpango wa “Uturuki isiyokuwa na Ugaidi”.
Alieleza kuwa mpango huo ni wa “kimkakati na kihistoria kulinda demokrasia yetu kutokana na vitisho vyote,” akiongeza kuwa ni ishara ya “msimamo dhidi ya majaribio ya kuleta ushawishi wa kikoloni katika kanda kwa kutumia mashirika ya kigaidi.”
Celik amesema mchakato huo, unaoungwa mkono na Rais Tayyip Erdogan kwa “uongozi thabiti wa nchi” na kuelekezwa na Tume ya umoja wa kitaifa ya bunge, Undugu na Demokrasia, “unaendelea kupata matokeo mazuri.”
Aliongeza kuwa Uturuki iko makini kwa majaribio yoyote yatakayochochea utovu wa usalama katika kanda, ikiwemo siasa, ujasusi na juhudi za operesheni za kudumaza mchakato huo.


















