| Swahili
AFRIKA
2 DK KUSOMA
Wafanyakazi wa UN wakimbilia Rwanda kukwepa machafuko DRC
Waasi wa M23 wanadai kuudhibiti mji wa Goma ulioko DRC.
Wafanyakazi wa UN wakimbilia Rwanda kukwepa machafuko DRC
Hatua hiyo inakuja saa chache baada ya waasi wa M23 kudai kuutwaa mji wa Goma, na kulazimu wakazi wa eneo hilo kuukimbia mji huo. /Picha: Reuters  / Others
27 Januari 2025

Mamia ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa pamoja na raia waishio Mashariki mwa DRC wamekimbilia Rwanda kukwepa machafuko hasa baada ya waasi wa M23 kutwaa mji wa Goma.

Picha za video zilizowekwa na Shirika la Habari la Rwanda kwenye mtandao wa X, zilionesha vikosi vya kijeshi vikisalimisha silaha zao kwa maafisa wa usalama wa Rwanda baada ya kuingia kwenye mpaka wa nchi hiyo ulioko kwenye wilaya ya Rubavu.

Hatua hiyo inakuja saa chache baada ya waasi wa M23 kudai kuutwaa mji wa Goma, na kulazimu wakazi wa eneo hilo kuukimbia mji huo.

Kikundi cha M23, kinachodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, wiki iliyopita kiliongeza mashambulizi katika eneo la Mashariki mwa DRC na kudhibiti maeneo nyeti.

Hata hivyo, madai hayo yamepingwa vikali na serikali ya Rwanda.

Wakuu wa EAC kuitisha kikao cha dharura

Rais wa Kenya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), siku ya Jumapili alitangaza juu ya uwepo wa kikao cha dharura ndani ya saa 48 zijazo, kujaribu kutafuta muafaka wa machafuko ndani ya DRC.

Ruto alithibitisha kuwa alifanya mazungumzo na Rais wa DRC Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda, huku wote wawili wakikubali kuhudhuria kikao hicho.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika