| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Antonio Guterres: Tanzania ni kielelezo cha amani Afrika, duniani
Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja siku chache, baada ya kadhaa za magharibi ikiwemo Marekani, kusema kwamba inatathmini upya uhusiano wake na Tanzania.
Antonio Guterres: Tanzania ni kielelezo cha amani Afrika, duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo./Picha:@mfa_tanzania
tokea masaa 2

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameimwagia sifa Tanzania, akiielezea kuwa ni kielelezo cha amani barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Kulingana na Mtendaji Mkuu huyo wa UN, Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani, akisisitiza kuwa dunia nzima, inalitazama taifa hilo kama mfano wa kuigwa.

Hata hivyo, Guterres, ambaye alikuwa akizungumza baada ya kupokea Ujumbe Maalumu kutoka Tanzania, Disemba 14, 2025, alisema kuwa sifa hiyo nzuri ya Tanzania, ilipitia majaribio wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, licha ya kufanikiwa kuyavuka.

Aidha, Guterres alisema kuwa anafurahishwa kuona Tanzania ikiendelea kuwa na umoja, licha ya changamoto hizo, akisisitizia umuhimu wa kuwa na mazungumzo ya kitaifa kutafuta suluhu ya vurugu baada ya Uchaguzi Mkuu.

Kulingana na Guterres, Umoja wa Mataifa upo tayari kutoa msaada kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya uvunjifu wa Amani, maarufu kama Tume ya Jaji Othman Chande.

Haya yanajiri baada ya jumuiya za kimataifa, ikiwemo nchi za magharibi ikiwemo Marekani, kusema kwamba inatathmini uhusiano wake na Tanzania.

Tanzania inashika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na askari wengi wanaoshiriki operesheni za kulinda amani zilizo chini ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu, Tanzania ilikuwa na jumla ya walinda amani 1,538 katika mataifa mbalimbali duniani, ikitanguliwa tu na Rwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Baadhi ya operesheni hizo ni pamoja na SAMIM ya nchini Msumbiji, MINUSCA ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, MONUSCO ya DRC, UNAMID Kusini mwa Darfur na UNIFIL ya nchini Lebanon.

CHANZO:TRT Afrika Swahili