| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
UN yawasihi Eritrea na Ethiopia kuheshimu makubaliano ya mpaka wa miaka 25 iliyopita
Eritrea na Ethiopia zilitia saini makubaliano ya Algiers baada ya majirani hao wawili kupigana vita vya umwagaji damu mwaka 1998-2000, na kusababisha vifo vya watu 70,000-80,000 kwa pande zote mbili.
UN yawasihi Eritrea na Ethiopia kuheshimu makubaliano ya mpaka wa miaka 25 iliyopita
Eritrea ilijitenga rasmi na Ethiopia mwaka 1993. / / AA
tokea masaa 17

Umoja wa Mataifa umezitaka Eritrea na Ethiopia kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Algiers uliokomesha rasmi uhasama kati ya mataifa hayo ya Pembe ya Afrika miaka 25 iliyopita, huku ukionya kwamba mvutano unaoibuka upya unaweza kuhatarisha amani ya kanda.

Mkataba wa Algiers ulisainiwa baada ya majirani hao wawili kupigana vita vikali kati ya mwaka 1998 na 2000, vita ambavyo vilisababisha vifo vya watu kati ya 70,000 na 80,000 kutoka pande zote.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa na Stephane Dujarric msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema kuwa “leo ni kumbukumbu ya miaka 25 ya Mkataba wa Algiers, mkataba muhimu wa amani uliokomesha mzozo wa mpaka kati ya Eritrea na Ethiopia na kuweka misingi ya mahusiano ya amani kati ya mataifa hayo mawili.”

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa mkataba huo uliweka “utaratibu wa kuweka alama na kuainisha mpaka wa pamoja” na pia “ulithibitisha upya misingi ya mamlaka kamili ya mataifa na ukamilifu wa mipaka yao,” kwa uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa.

“Katika hatua hii muhimu ya kihistoria, Katibu Mkuu anarejea kusisitiza uungaji mkono thabiti wa Umoja wa Mataifa kwa Mkataba wa Algiers,” taarifa ilisema. “Miaka saba iliyopita, viongozi wa nchi zote mbili walirudia dhamira yao ya kuendeleza amani kupitia tamko la pamoja, ushahidi wa nguvu ya mazungumzo na ushirikiano.”

Dhamira ya kuendeleza amani’

Wakati huu ambapo mvutano unaonekana kuongezeka tena, Guterres amezitaka “Eritrea na Ethiopia kuimarisha dhamira ya amani ya kudumu na kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa mipaka kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Algiers, na kuongeza juhudi za kujenga uhusiano mwema wa kijirani.”

Kiongozi huyo wa UN pia amezihimiza pande zote mbili “kuendelea kushirikiana na washirika wa kikanda na kimataifa kuendeleza ushirikiano wa maendeleo kwa manufaa ya wote.”

Baada ya vita vya 1998–2000, Tume ya Kimataifa ya Mipaka iliamua kwamba mji wa Badme—eneo lililokuwa chanzo kikuu cha mzozo—ni la Eritrea. Pia iliamua kuwa Eritrea ilipaswa kulipa fidia Ethiopia kwa shehena kubwa za bidhaa za Ethiopia zilizotaifishwa katika Bandari ya Assab.

Eritrea ilijitenga rasmi na Ethiopia mwaka 1993.

CHANZO:AA