Siku ya Jumatatu, Uingereza ilianza kutekeleza marufuku nchini humo ya matangazo ya vyakula visivyo na afya (junk food) kwenye televisheni na mtandaoni, kama sehemu ya juhudi za serikali kukabiliana na ongezeko la unene kwa watoto.
Chini ya sheria mpya, vyakula na vinywaji vinavyokadiriwa kuwa na mafuta mengi, chumvi nyingi na sukari nyingi (HFSS) havitaruhusiwa kutangazwa kwenye televisheni kabla ya saa 3 usiku (9 pm kwa saa za Uingereza), wala kutangazwa kupitia matangazo ya kulipiwa mtandaoni wakati wowote.
“Watoto watalindwa dhidi ya kuonyeshwa kwa kiasi kikubwa matangazo ya vyakula visivyo na afya kwenye televisheni na mtandaoni,” Wizara ya Afya ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.
Wizara hiyo iliongeza kuwa kanuni hizi zinatarajiwa kupunguza idadi ya watoto wanaoishi na unene kupita kiasi kwa 20,000, na kuleta faida za kiafya za takribani pauni za Uingereza bilioni 2 (sawa na dola bilioni 2.68) kwa muda.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, asilimia 22.1 ya watoto nchini Uingereza wana uzito kupita kiasi au unene wanapoanza shule ya msingi, na idadi hiyo huongezeka hadi asilimia 35.8 wanapomaliza shule ya msingi.
Ongezeko la kisukari miongoni mwa watoto
Waziri wa Afya ya Umma, Ashley Dalton, alisema kuwa kuzuia matangazo ya vyakula visivyo na afya kabla ya saa 3 usiku na kupiga marufuku matangazo ya kulipiwa mtandaoni kutapunguza kuonekana kwa wingi wa vyakula visivyo na afya, na kusaidia kufanya chaguo bora la kiafya kuwa rahisi kwa wazazi na watoto.
Katharine Jenner, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Obesity Health Alliance’, aliipongeza hatua hiyo akisema kuwa hatimaye watoto watalindwa dhidi ya matangazo mabaya zaidi ya vyakula visivyo na afya.
Colette Marshall, mkurugenzi mkuu wa shirika la Diabetes UK, alisema kuwa haja ya kuimarisha afya ya watoto “imefanywa kuwa bora zaidi,” huku ugonjwa wa kisukari ukiendelea kuongezeka miongoni mwa vijana.
“Unene kupita kiasi ni sababu kubwa ya hatari ya kupata kisukari, na ugonjwa huu unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa vijana, ukiwaweka katika hatari ya matatizo makubwa kama matatizo ya figo na magonjwa ya moyo,” alisema.














