Rais wa Marekani Donald Trump amewataka waandamanaji wa Iran kuendelea “kuandamana na kuchukua udhibiti wa taasisi,” akisema kuwa “msaada unakuja,” huku akiwaonya maafisa wa Iran kwamba watalipa gharama kubwa.
“Wazalendo wa Iran, endeleeni kuandamana, chukueni udhibiti wa taasisi zenu!!! Muhifadhi majina ya wauaji na wanyanyasaji. Watalipa gharama kubwa,” Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social siku ya Jumanne.
Aliongeza kuwa amesitisha mikutano yake yote na wanadiplomasia wa Iran.
“Nimesitisha mikutano yote na maafisa wa Iran hadi mauaji ya kipuuzi ya waandamanaji yakome. Msaada unajuka. MIGA!!! (Ifanye Iran iwe kubwa tena)”
Trump alitumia kauli mbiu yake maarufu ya ‘Make America Great Again’, lakini mara hii ametumia neno Iran badala ya Marekani.
Siku ya Jumatatu, Ikulu ya White House ilisema rais wa Marekani “ana nia” ya kutafuta uwezekano wa kufanya mazungumzo ya diplomasia na Iran.
Msemaji Karoline Leavitt alisema Trump “haogopi” kutekeleza vitisho vyake vya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran iwapo waandamanaji watashambuliwa na vikosi vya usalama, lakini akasema anapendelea zaidi kufuata diplomasia na nchi hiyo.
Maafisa wa Iran wameituhumu Marekani na Israel kwa kuunga mkono kile wanachokiita “waasi wenye silaha,” ambao wamedaiwa kutekeleza mashambulizi kadhaa katika maeneo ya umma kote nchini.
Hakuna takwimu rasmi za vifo, lakini shirika moja la haki za binadamu lenye makao yake Marekani linakadiria kuwa idadi ya waliokufa imefikia angalau 646, wakiwemo maafisa wa usalama na waandamanaji, huku zaidi ya 1,000 wakijeruhiwa.
Shirika hilo pia liliripoti kuwa angalau watu 10,721 wamekamatwa katika maandamano yaliyofanyika katika maeneo 585 kote nchini, ikiwemo miji 186 katika majimbo yote 31.






















