Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema kuwa hakuna mgonjwa wa Uviko-19 aliyeripotiwa kulazwa, bali imewataka ananchi kuendela kuchukua tahadhari na kufuatilia ushauri wa kitaalamu ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama ilivyoelezwa katika taarifa kwa umma ya Mganga Mkuu wa serikali hivi karibuni.
Kulingana na Waziri wa Afya nchini humo, Mohammed Mchengerwa, serikali ya Tanzania bado inaendelea kufuatilia kwa ukaribu juu ya mienendo ya magonjwa mbalimbali kama kipindu pindu, Dengue na UVIKO-19 hususani katika kipindi cha mvua.
“Napenda kuwahakikishia wananchi na Watanzania wote serikali yenu ipo makini na inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maambukizi ya UVIKO-19 nchini na kimataifa, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na wataalamu wa afya ili kulinda afya binafsi na ya jamii kwa ujumla,” amesema Mchengerwa.
Waziri huyo, alisisitiza kuwa, ni jukumu la Wizara kuhakikisha linatoa mwenendo wa magonjwa mbalimbali hasa ya mlipuko ili kuhakikisha wananchi wanachukua tahadhari ya ugonjwa husika.
Februari 25 mwaka huu, Wizara ya Afya nchini humo, ilitoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya mlipuko nchini, ikiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, Homa ya Dengue na Kipindupindu, huku ikitoa tahadhari na wito kwa wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa jijini Dodoma, Wizara hiyo ilieleza kuwa katika kipindi cha karibuni kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na Uviko-19.














