Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemaliza ziara yake ya New York katika kikao cha 80 cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mikutano mingine jijini Washington na Rais wa Marekani Donald Trump, akieleza kuwa safari hiyo ilikuwa “nzuri, yenye tija, na ya kihistoria” kwa diplomasia ya Uturuki.
Erdogan amesisitiza kuwa mkutano wa mwaka huu wa UNGA uliangazia zaidi hali ilivyo Gaza. “Mauaji ya halaiki ya Gaza na suala zima la Palestina limejadiliwa sana katika Mkutano wa Baraza Kuu la mwaka huu,” alisema, akieleza kuwa Uingereza, Ufaransa, na mataifa mengine kumi ya Magharibi yametangaza kutambua Palestina.
“Maamuzi haya ya kutambua, hasa kutoka kwa wanachama wawili wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni ya kihistoria. Kwa hatua hizi, idadi ya nchi ambazo zinatambua Palestina imepita 150. Kuungwa mkono kwa suluhu la mataifa mawili kunaongezeka zaidi, lakini jamii ya kimataifa lazima ichukuwe hatua madhubuti kwa hili kutimia,” Erdogan alieleza.
Alieleza kuwa “hatua mbaya na sera za ukaliaji” za Israel zinazolenga kukwamisha juhudi kama hizo, akiongeza kuwa yeye mwenyewe alizungumzia suala hilo la Gaza katika hotuba yake kwenye mkutano wa UNGA, kwenye kikao cha pamoja na Trump, na kwenye mkutano mwingine wa ngazi ya juu ulioratibiwa na wanachama wenza Ufaransa na Saudi Arabia. “Tutaendeleza juhudi zetu kwa suala hili,” alisema.
Rais wa Uturuki pia alisisitiza misimamo ya Uturuki kuhusu suala la Kupro, Syria, na vita vya Urusi na Ukraine, na pia kueleza kuhusu juhudi za Uturuki za kufikishia watu misaada na kuleta upatanishi, ikiwemo makubaliano ya Nafaka ya Bahari Nyeusi na kubadilishana wafungwa.
Lengo la kufikisha biashara ya dola bilioni 100 kwa mataifa mawili
Kuhusu agenda ya biashara kwa mataifa mawili, Erdogan alieleza kuwa mkutano wake na Trump uliangazia biashara, ushirikiano wa masuala ya ulinzi, na usalama katika kanda. Viongozi hao wawili walithibitisha kuhusu lengo lao la kufanya biashara ya dola bilioni 100, huku Erdogan akieleza kuwa ushuru na hatua zingine za kufanikisha biashara zilijadiliwa.
Ushirikiano katika masuala ya ulinzi, aliongeza, yalizungumziwa “kwa mtazamo wenye tija.” Sehemu kubwa ya mazungumzo ilikuwa kuhusu Gaza, huku Erdogan akisisitiza kuwa pande zote mbili zilikuwa na dira ya pamoja ya kuzuia umwagikaji damu na kuelekea katika hatua ya kupata amani ya kudumu.
“Tulipokelewa vizuri katika Ikulu ya White House. Mazingira yalikuwa ya uwazi na yenye tija ,” Erdogan aliwaambia waandishi wa habari. “Rais Trump ni mwanasiasa ambaye anazungumza wazi, na mazungumzo yetu yaliakisi hali hiyo. Ziara hii haiwezi kuharibia na watu kuharibu sifa. Itakuwa na matokeo chanya kwa uhusiano wa Uturuki na Marekani.”
Kuhusu Gaza, Erdogan alisema alimueleza Trump moja kwa moja kuhusu hali mbaya ya watu huko. “Tulizungumza kuhusu namna gani tutaharakisha usitishwaji wa mapigano, alafu baadaye amani ya kudumu. Kulikuwa na maoni yaliyolingana.”
“Suluhu ya mataifa mawili bado ndiyo mfumo mzuri wa kupatikana kwa amani endelevu katika kanda hiyo. Mauaji ya watoto, wanawake, na raia wasio na hatia hayawezi kutumiwa kama kisingizio cha usalama,” aliongeza, akiapa kuwa Uturuki itaendeleza kulifanya suala hilo kuwa agenda ya kimataifa “hadi pale amani ya haki na ya kudumu itakapopatikana.”
Erdogan pia alizungumzia kuhusu picha za madhila wanayopitia watu alizozionesha wakati wa hotuba yake ya UNGA, ikiwemo utapiamlo wa watoto wa Gaza. “Picha hizo zinazungumza pale ambapo maneno hayawezi kuzungumza,” alisema, akiongeza kuwa Israel inaendelea kutengwa zaidi. “Kutambuliwa kwa Palestina na nchi zaidi na zaidi kunaonesha kuwa watu bado wana utu.”
Uhuru wa mipaka ya Syria
Kuhusu masuala ya kanda, Erdogan amesisitiza kuunga mkono uhuru wa mipaka ya Syria na kueleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi ya Israel kote Mashariki ya Kati, ikiwemo Syria, Lebanon, na Yemen. Alithibitisha katika mkutano wake na Rais wa Syria Ahmed al Sharaa jijini New York, akisisitiza utayari wa Uturuki kushirikiana katika ujenzi upya wa Syria na kusisitiza kuwa “makundi ya kigaidi hayana nafasi katika mustakabali wa Syria.”
Pia alizungumzia kuhusu kuimarika kwa uhusiano wa Uturuki na Misri, akieleza kuhusu mazoezi ya pamoja ya majeshi ya wanamaji katika bahari ya Mediterania Mashariki baada ya miaka 13. Alieleza kuwa ushirikiano wa Misri na Libya unaimarika, akisisitiza dhamira ya Uturuki kulinda haki zake wakati ikitafuta muafaka wa “faida kwa pande zote” katika suala la raslimali za bahari ya Mediterania.
Kuhusu suala la Kupro, Erdogan alisisitiza kuwa “mfumo wa shirikisho umekwisha” na kwamba suluhu pekee ya kweli ni kutambuwa mataifa mawili huru. Alisisitiza kuwa uchaguzi unaotarajiwa katika Jamhuri ya Uturuki ya Kupro Kaskazini hautabadilisha msimamo wa Uturuki.
Mwisho, Erdogan alisisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa katika kipindi ambacho kuna changamoto kutoka nje, akikumbuka msisitizo wake wa awali wa kuimarisha “masuala ya nyumbani.” Alieleza dhamira ya kuwa na nchi ya Uturuki ambayo mustakabali wake “hautakuwa na ugaidi” huku ikiendelea kuimarisha masuala ya ulinzi, teknolojia, na uchumi.
“Sera ya mambo ya nje ya Uturuki inaangazia amani zaidi. Tunajuwa kuwa hakuna mtu anayepoteza palipo na amani ya haki. Hadi pale umwagikaji damu utakapomalizika, Uturuki itaendelea na mapambano,” Erdogan alihitimisha.