Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemueleza Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kuwa “mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Gaza, yameingia hatua mpya” yakiendelea kuhatarisha utulivu wa kikanda, kulingana na taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Mapema wiki hii, Israel ilifanya shambulio dhidi ya mji wa Gaza, katika sehemu yenye watu wengi.
Erdogan pia alitanabaisha shambulio la Israel dhidi ya Qatar mapema mwezi huu, akiliita “ushahidi kuwa haliathiri watu wa Palestina peke yake, bali utulivu wa kikanda.”
Kulingana na kiongozi huyo wa Uturuki, idadi ya viongozi wa dunia wenye kulaani yanayofanywa na Israel, inazidi kukua, akisisitiza kuwa Uturuki ilikuwa inafanya kila jitihada kuongeza shinikizo la kimataifa.
Rais Erdogan aliahidi kuendeleza vuguvugu la “Palestina katika kila jukwaa.”
Erdogan alisema kuwa kipaumbele cha Uturuki ni kuhakikisha mapigano na janga la kibinadamu linamalizika, akiahidi kuwa nchi yake itakuwa “sauti ya Palestina” katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Rais aligusia pia haja ya jumuiya ya Kiislamu ulimwenguni kuungana na kukabiliana na tishio la Israel, na kuongeza kuwa, kuanzishwa kwa umoja wa kisiasa wa Palestina, utahuisha jitihada hizo.
Kulingana na Erdogan, Uturuki itaendelea kuunga mkono jitihada hizo,” ilisomeka sehemu ya andiko katika ukurasa wa X wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Mwezi uliopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilibatilisha vivali vya kusafiri vya wanachama wa chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) na Mamlaka ya Palestina, kuelekea Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi Septemba.
Wizara hiyo ilisema katika taarifa yake kuwa: “Kulingana na sheria za Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio anazuia na kubatilisha vibali hivyo kwa wanachama wa PLO na Mamlaka ya Palestina, kuelekea baraza hilo.”
Mataifa kadhaa ya kimagharibi, ikiwemo Ufaransa na Uingereza, wametangaza mpango wa kulitambua taifa la Palestina wakati wa vikao vijavyo vya Umoja wa Mataifa.
Mwezi Agosti, Israel iliidhinisha mpango wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa kuitwaa Gaza, wakianzia na mji wa Gaza.
Siku ya Jumanne, Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu suala la kutwaliwa kwa eneo la Palestina, lilithibitisha kuwa Israel ilikuwa imetekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza.