Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema hotuba yake katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) itajikita kwenye "mauaji" yanayofanywa na Israel huko Gaza, akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kulinda Wapalestina na kuendeleza suluhisho la mataifa mawili.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Ataturk mjini Istanbul kabla ya kuelekea New York siku ya Jumapili, Rais Erdogan alisema, "Katika hotuba yangu kwenye Umoja wa Mataifa, nitazungumzia mateso yanayoendelea Gaza, na juhudi za Uturuki katika kulinda utulivu wa eneo hili."
Aliongeza kuwa mkutano wa UNGA wa mwaka huu utakuwa tofauti na ya awali, kwani "mataifa mengi yatatambua Dola ya Palestina."
Rais huyo alieleza matumaini yake kwamba kutambuliwa kwa Palestina kwa kiwango kikubwa kutasaidia "kuharakisha utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili," akiongeza kuwa haki na usalama wa Waturuki wa Cyprus pia vitakuwa sehemu ya ajenda yake.
Erdogan alisema atakutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, wakati wa mkutano huo kujadili ushirikiano katika biashara na sekta ya ulinzi, huku akisisitiza kwamba "muundo wa sasa wa Umoja wa Mataifa hautoshi kutekeleza majukumu yake."
Rais wa Uturuki pia alisema atakutana na Rais wa Syria, Ahmed al Shara, na Waziri wa Mambo ya Nje, Asaad Al Shaibani, huko New York, ikiwa ni mara ya kwanza kwa uongozi wa Syria kuwakilishwa katika UNGA kwa miongo kadhaa.
"Ndugu na dada zetu wa Syria wamelipa gharama kubwa kwa ajili ya uhuru wao. Tunatumaini UNGA itachangia uhuru wa Syria," alisema, akiongeza kuwa Uturuki inataka "amani katika kila sehemu ya eneo letu."