Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amefanya mazungumzo ya simu na mawaziri wenzake wa Saudi Arabia na Misri kuhusu hali ya Gaza.
Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki, Fidan alifanya mazungumzo tofauti na Waziri wa Mambo wa Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan na Badr Abdelatty, wa Misri.
Mazungumzo yao yaliangazia suala la Gaza na maandalizi ya Baraza la Umoja wa Mataifa ambalo litakaa wiki ijayo, vilisema vyanzo hivyo.
Mapema siku hiyo, Fidan alisema kuwa Uturuki imekuwa ni mfadhili wa amani, utulivu na haki, akisisitizia nafasi ya Ankara katika kuzuia na kumaliza migogoro.
"Nguvu yetu ya kidiplomasia ina nafasi muhimu ya kuzuia na kumaliza machafuko. Leo hii, Uturuki imekuwa mfadhili wa amani, utulivu na haki katika kanda yetu kutokana na diplomasia ya mkuu wetu wa nchi,” alisema Hakan Fidan.
Akiipiga kijembe Isreal, Fidan alisema “Uhalali wa sera za Israel na ukandamizaji wake wa Kisayuni umewekwa wazi, huku vuguvugu la Kipalestina likizidi kushika kasi.”
"Leo hii, kutoka Ukraine hadi Syria, kutoka eneo la Caucasus hadi pembe ya Afrika, Uturuki imedhihirisha nafasi yake katika mabadiliko ya kikanda,"alisema Fidan, na kuongezea shukrani kwa uongozi thabiti wa Rais Recep Tayyip Erdogan.
Diplomasia ya Uturuki
Akigusia mabadiliko ya kidiplomasia, Fidan alisema uwepo wa diplomasia ya kisasa, tamaduni za karne ya 17 na 18, zimefungua njia kwa michakato mipya.
Pia, alibainisha kuwa diplomasia imepitia mabadiliko kadhaa kutoka mikataba ya muda mfupi hadi kufikia mahusiano thabiti.
"Tunaendelea kujitanua kimataifa. Tukiwa na balozi 263, kwa sasa tunashika nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na mtandao mkubwa wa kidiplomasia," aliongeza.
Kulingana na Fidan, kuna jeografia mpya, changamoto na fursa mpya huko mbele, huku akisisitiza umuhimu wa diplomasia imara.
Alibainisha kuwa diplomasia ya Uturuki imekita mizizi kwenye tamaduni za karne na karne.
Kulingana na Fidan, kumbukumbu zote za wizara hiyo, zinawakilisha kumbukumbu ya taifa la Kituruki.